Na Mwandishi wetu
Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Rufiji wamepatia vifaa saidizi ikiwemo Viti mwendo 45 ambavyo vimetolewa na Mbunge wa Jimbo hilo mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa TAMISEMI ikiwa ni sehemu ya uwezeshaji kwa kundi hilo kuendelea kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.
Akikabidhi vifaa hivyo wakati wa mafunzo ya watu wenye ulemavu sambamba na mwendelezo wa programu za tamasha la kumbukumbu ya Bibi Titi Mohammed katika Ukumbi wa Ikwiriri Wilaya ya Rufiji, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaasa kutunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa manufaa ya ambapo pia alishiriki chakula cha pamoja na watu wenye ulemavu wakati wa mafunzo hayo.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa kundi hilo limekuwa likikutana na changamoto nyingi ikiwamo kudharauliwa, kubaguliwa, kutoaminiwa na hata kunyanyaswa kutokana na hali zao na kuitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa na kuwaficha watu wenye ulemavu badala yake wawaibue na kuwaunganisha na fursa mbalimbali katika jamii.
Naibu Waziri huyu akikabidhi vifaa hivyo amemshukuru mbunge huyo kwa kuendelea kuwapenda na kuwajali watu wenye ulemavu na kueleza kuwa zoezi la kubaini takwimu za watu wenye ulemavu wote pamoja na mahitaji yao kulingana na aina ya ulemavu walio nao lengo ni kuweza kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mahitaji yao.
“Kipekee nampongeza Mbunge wenu hapa Rufiji Mhe. Mchengerwa kwa namna anavyowapigania na kujali mahitaji yenu na leo ameniomba niwe mgeni rasmi na kukabidhi vifaa hivi, tuendelee kumuunga mkono mbunge wetu kwa moyo wake wa kizalendo kwa wana Rufiji,” alisisitiza Naibu Waziri huyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali na inatambua kundi la Watu wenye ulemavu.
“Serikali imekuwa ikiandaa na kusimamia programu mbalimbali za uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kama vile kutenga nafasi maalum za ajira, kusisitiza uwekaji wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu katika ofisi na taasisi mbali mbali za umma, kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu,”Amesema Mhe. Ummy.
Pia ameeleza kwamba kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 -2025 ibara ya 94 na 95 imeweka bayana na kuielekeza Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa watu wenye ulemavu ili waendelee kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.
“Mafunzo haya yatakayotolewa yasaidie kutujenga na kutuwezesha kutambua na kupambanua masuala mbalimbali yanayohusu Watu wenye ulemavu na hii iwe ni fursa na chachu ya kuongeza ushiriki wa kila mmoja wetu katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” Ameeleza Mhe. Ummy.
Aidha Mhe. Ummy aliwakumbusha adhma ya Serikali ni kuhakikisha watu wenye ulemavu nchini wanaendelea kupatiwa huduma zote muhimu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo huku akieleza kuwa waendelee kujiamini sababu Serikali yao inawajali na kuthamini sana mchango wao katika Taifa.
“Mhe Samia Suluhu Hassan ameendelea kutujali sisi watu wenye ulemavu hivyo tusiwe wanyonge na tuendelee kumuunga mkono katika kujiletea maendeleo yetu ya kila siku.
Social Plugin