Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameielekeza Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuona namna ya kushirikiana na Wadau katika kuanzisha programu zitakazowezesha huduma za ustawi wa jamii kuwafikia wananchi katika ngazi ya kata na kijiji.
Waziri Gwajima ametoa maelekezo hayo wakati wa Mahafali ya 47 ya Taasisi hiyo Disemba 08, 2023 Dar Es Salaam.
Amesema kutokana na upungufu wa Maafisa ustawi wa Jamii hasa, katika ngazi ya Kata na Kijiji Taasisi inapaswa kuwa na Programu hizo ikizingatiwa kwamba, inazalisha Wataalamu wa Fani ya Ustawi wa Jamii ambayo ni Kada muhimu katika utekelezaji wa mipango ya Wizara.
Waziri Dkt. Gwajima amemshukuru Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri Wahadhiri 58 kwa Taasisi hiyo hali itakayoongeza nguvu kazi na kuleta tija katika kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi.
"Ikumbukwe Serikali imewekeza sana katika sekta ya elimu hivyo, kama Chuo nanyi hamna budi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha mnatoa wahitimu walioiva vizuri kwa kutumia rasilimali mlizonazo". amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha ameipongeza Taasisi kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia hasa kusomesha watumishi kwenye ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) na kuweka mkazo kwenye mafunzo ambayo yanalenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri.
Amebainisha pia Serikali kuweka miongozo mbalimbali na sasa inaandaa muongozo wa utoaji wa huduma za ustawi wa jamii zitakazowezesha watu binafsi na Taasisi kutoa huduma hizo na kutoa wito kwa wahitimu kutumia fursa hiyo kuanzisha huduma za ustawi wa jamii ambazo zinahitajika kwa kiasi kikubwa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi hiyo Mhe. Sophia Simba ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa uwekezaji katika sekta ya elimu ambapo imewezesha Taasisi kufanya juhudi kuboresha mazingira ya kufundishia huku nguvu kubwa ikiwa kwenye TEHAMA, malazi, kumbi za mihadhara na mafunzo.
Mhe. Sophia ameeleza pia kuanzishwa kwa Kitengo cha kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuboresha huduma kwa wanafunzi hao.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni, awali ameeleza kuwa Taasisi hiyo yenye wanafunzi 5765 hadi sasa, imeendelea kuboresha mitaala kwa kuzingatia zaidi mahitaji ya Jamii hali iliyochangia kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kutoka 2001 mwaka 2022/23 hadi wanafunzi 2114 mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 5.3.
Social Plugin