Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kimenuka Mbaya! WANANCHI WABOMOA LAMI BARABARA YA SHINYANGA - MWANZA BALAA LA AJALI BUGWETO

 
Tazama Video 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Ni tukio la aina yake au maamuzi magumu ya hatari! Hii ni baada ya wananchi wenye hasira kali eneo la Bugweto Manispaa ya Shinyanga kubomoa/kuchimba lami katika Barabara kuu ya Shinyanga - Mwanza wakishinikiza kuwekewa vizuia mwendo (Matuta/Bumps) katika njiapanda ya Bugweto eneo ambalo wananchi wanasema limekuwa sugu kwa ajali za mara kwa mara hali inayosababisha vifo na majeruhi.

Tukio la kubomoa barabara limetokea saa chache baada ya wananchi hao kulazimika kufunga barabara kuu ya Shinyanga - Mwanza baada ya leo Jumatano Januari 31,2024 watu wawili waliokuwa wamepanda kwenye baiskeli kugongwa na gari na kusababisha kifo cha Daudi Kulwa Mwandu (25) mkazi wa Bugweto na mwingine Athuman Mtatiro Wambura (33) mkazi wa Tambukareli kujeruhiwa.

Wakizungumza na Malunde 1 blog baadhi ya wananchi hao wamedai ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwenye barabara hiyo zikisababishwa na mwendokasi unaosababishwa na baadhi ya madereva wa magari na kupelekea vifo na majeruhi ambapo leo pekee asubuhi ajali tatu zimetokea.

Baadhi ya wananchi wamedai kuwa ukosefu wa kizuia mwendo (matuta) kwenye barabara hiyo na baadhi ya madereva kutofuata sheria za usalama barabarani imekuwa chanzo cha kusababisha vifo vitokanavyo na ajali.

Malunde 1 blog imefika eneo la tukio na kushuhudia Maafisa kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga wakitengeneza Matuta (Bumps) katika barabara hiyo baada ya wananchi kubomoa/kuchimba lami hiyo huku askari Polisi wakiimarisha ulinzi na usalama katika barabara hiyo.

Awali Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi amefika eneo la tukio na kuzungumza na wananchi hao ambapo amesema wataendelea kuimarisha doria za usalama barabarani katika eneo huku katibu tawala wilaya ya Shinyanga Said Kitinga amefika na kuchukua hatua kwa kuzielekeza mamlaka husika.

Soma pia

Maafisa kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga wakitengeneza Matuta (Bumps) katika barabara hiyo baada ya wananchi kubomoa/kuchimba lami hiyo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com