TAWIRI NA MUENDELEZO WA TAFITI UGONJWA WA TWIGA ULIOATHIRI ASILIMIA 62 YA TWIGA KATIKA HIFADHI YA TAIFA RUAHA



Taasisi ya Utafiti wa  Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) inaendelea kufanya  tafiti zaidi juu ya madhara na matibabu ya ugonjwa wa ngozi wa Twiga ambao  matokeo ya awali yameonyesha maeneo yanayoathirika ya viungio kwenye miguu (magoti) hususan miguu ya mbele, kuna vimelea vya bakteria, virusi na fangasi.

Akizungumza wakati wa ufuatiliaji wa matibabu ya ugonjwa huo katika hifadhi ya Taifa Ruaha, Dkt. Julius Keyyu ambaye ni  Mkurugenzi wa Utafiti  TAWIRI,  amesema ugonjwa wa ngozi wa Twiga uliogundulika katika hifadhi  ya Taifa  Ruaha mwaka 2000 ni tofauti na ugonjwa wa ngozi wa Twiga katika nchi nyingine duniani 

"Tumefuatilia ugonjwa huu kwa nchi nyingine duniani na kubaini upo tofauti na hapa nchini", amebainisha  Dkt. Keyyu

Dkt. Keyyu amesema asilimia  62% ya Twiga waliopo hifadhi ya  Taifa Ruaha wana ugonjwa wa ngozi ambao pia, umeonekana kwa kiwango kidogo katika hifadhi za Taifa za Tarangire na Serengeti, na tafiti za awali zimeonesha madhara ya ugonjwa huo ni pamoja na Twiga wenye ugonjwa kutembea kwa  kuchechemea, hivyo kushindwa kukimbia wanapofukuzwa na wanyama wawindao pia hutembea umbali mdogo kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi ukilinganisha na Twiga wasio na ugonjwa. 

Dkt. Keyyu amesema kwa sasa TAWIRI inaendelea na ufuatiliaji wa matibabu ya ugonjwa huo ili kubaini kisababishi asili cha ugonjwa (primary agent) na kupata matokeo ya kushauri nini kifanyike ili kudhibiti ugonjwa huu wa ngozi wa Twiga na kuhakikisha mnyama huyu ambaye ni nembo ya taifa anazidi kuwepo.

Ikumbukwe  utafiti  wa  ugonjwa  huu wa ngozi  wa  twiga  unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) uliopo chini  ya  Wizara  ya  Maliasili  na  Utalii  na jukumuu la TAWIRI  ni kufanya  tafiti .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post