Na mwandishi wetu, Tanga
Baada ya kukamilika miradi ya maboresho katika bandari ya Tanga, kumepelekea tija kubwa kuonekana katika nyanja tofauti ikiwemo kuongezeka kwa shehena na meli zinazohudumiwa katika bandari hiyo jambo ambalo linachangia ongezeko la mapato.
Hayo yamesemwa leo Jumanne tarehe 23 Januari, 2024 na Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema, miradi ya maboresho katika bandari hiyo ilitekelezwa kwa awamu mbili na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 429.1.
Kwa upande shehena, Meneja Mrisha ameeleza kuwa, bandari ya Tanga baada ya maboresho hayo sasa itakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.
Bandari ya Tanga kabla ya maboresho, kwa mwaka ilikuwa na uwezo wa kuhudumia tani 750,000 lakini baada ya maboresho bandari ya Tanga itahudumia hadi tani 3,000,000 kwa mwaka"
Ameendelea kwa kusema kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 (mwezi Julai hadi Desemba) bandari ya Tanga tumeweza kuhudumia tani 572,000 ambapo ni kiwango kikubwa ukilinganisha na kipindi kama hiko kwa mwaka uliopita wa fedha ambapo tuliweza kuhudumia tani 490,000 pekee" alisema Meneja Mrisha na kuongeza kuwa
"Katika mwaka wa fedha 2022/2023, bandari ya Tanga tuliweza kuhudumia tani 987,000 kiwango kikubwa kuliko mwaka wa fedha 2021/2022 tulipoweza kuhudumiwa tani 870, 000. Kwa maboresho yaliyofanyika, tunaweza kusema kwamba bandari ya Tanga imefunguka na kuzaliwa upya"
Kwa upande wa kuhudumia meli, Meneja wa Bandari hiyo amebainisha kuwa, wameweza kuvuka lengo kwa kuhudumia meli nyingi zaidi ikiwa ni mara mbili zaidi katika kipindi cha nusu mwaka huu wa fedha ikilinganishwa na kipindi kama hiko katika mwaka uliopita wa fedha.
"Lengo letu la katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2023 lilikuwa ni kuhudumia meli 110, lakini tumeweza kuhudumia meli 122 tumevuka lengo kwa 11% lakini kipindi kama hiko mwaka 2022/23 tuliweza kuhudumia meli 110 pekee" alisisitiza Mrisha
Baada ya maboresho kukamilika katika bandari ya Tanga, faida lukuki zimeweza kupatikana ikiwemo uharaka katika kuhudumia meli, idadi ya meli kuongezeka, gharama za uendeshaji kupungua, na mapato kuongezeka.
Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa katika bandari ya Tanga iliyojengwa katika miaka ya 1890's ni pamoja na kuongeza upana wa mlango bahari, sehemu ya kuingia na kutoka meli (entrance Channel) kwa mita 73, kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi mita 13, kuongeza sehemu ya kugeuzia meli (turning base) kutoka mita 3 hadi mita 13, kununua vifaa vya vya bandari ikiwemo mobile harbour crane mbili zenye uwezo wa kubeba tani 100 kila moja, forklift za tani 50 moja, forklift ya tani 16,forklift za tani 5 mbili, terminal tractora mbili, Rubber Tyre Gantry Crane (RTG) moja, spreaders za futi 40 mbili na spreaders za futi 20 mbili.
Social Plugin