Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Alexius Kagunze
#Asema baadhi ya wazazi walichanganya tu Fomu
#Wazazi wapewa pesa zao
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Alexius Kagunze ameagiza shilingi 4,475,000/= zilizolipwa kimakosa na wazazi wa wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga (Shinyanga Girls Secondary School) iliyopo kata ya Ndembezi zirudishwe kwa wazazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Januari 20,2024 Mwl. Kagunze amesema maagizo hayo ameyatoa kwa uongozi wa shule na maafisa elimu wilaya na kata kwamba wasimamie kuhakikisha fedha zote zinarejeshwa kwa wazazi.
“Nimeagiza wazazi wote ambao kimakosa walijikuta wamechukua fomu ya kujiunga kidato cha tano kwa shule za bweni badala ya fomu ya kujiunga kidato cha kwanza warejeshewe fedha zao shilingi 80,000/= (mchanganuo ni shilingi 65,000/= kwa ajii ya uendeshaji wa shule, Tahadhari 5,000, nembo ya shule 5,000/= na kitambulisho cha shule 5, 000/= tayari fedha zao jumla shilingi 4,475,000/= zimetolewa kwenye akaunti ya shule na tayari wazazi wameanza kurudishiwa fedha zao”,ameeleza Mwl. Kagunze.
“Maafisa elimu wilaya na kata wasimamie kuhakikisha kwamba fedha zote zirejeshwe kwa wazazi na risiti zote nizione na kama ni SMS za miamala ya simu nizione ili kumaliza mkanganyiko huo uliotokea. Tayari baadhi ya wazazi wamekiri kupokea fedha walizochanga ambapo kwa wale waliopo ndani ya mkoa wa Shinyanga wamefika shuleni wakachukua na wameshukuru kwa sababu kwa sasa elimu ni bure, Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga hii shule kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.1 na elimu ni bure kwa wanafunzi wote”,ameongeza Kagunze.
Akifafanua kuhusu mkanganyiko uliojitokeza, Mwl. Kagunze amesema umetokana na baadhi ya wazazi kuchanganya fomu ya kujiunga kidato cha tano na fomu ya kujiunga kidato cha kwanza ambapo baadhi ya waliochanganya ndiyo wale baadhi yao wakajikuta wanalipia shilingi 80,000/= ambayo inapaswa kulipwa na wazazi wa wanafunzi wa kidato cha tano ambao walishalipa mwaka 2023 na wanaendelea na masomo.
“Nimeona kwenye moja ya vyombo vya habari vikitangaza kwamba wazazi wamechangishwa fedha shilingi 80,000/= kwenye shule yetu ya Sekondari ya wasichana Shinyanga, katika kufuatilia hilo jambo ambalo limeenea kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii, nikafuatilia zaidi nikagundua kwamba wapo baadhi ya wazazi waliweza kulipa shilingi 80,000/= ya mchango ndani ya shule wamejikuta wakilipa kwa sababu shule hii ni mpya ilianza mwaka 13.08.2023 ambapo shule ilianza na kidato cha tano na kwa mujibu wa maelekezo walichangia shilingi 80,000/=”,ameeleza.
“Hiyo fomu huwekwa kwenye Tovuti za Wizara hata shuleni haipo, mtoto anapofaulu anaingia kwenye mtandao anachukua fomu anaona mahitaji yote ya shule. Sasa wazazi wa mwaka huu wa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza kwa sababu kila mwaka fomu inaweza kuboreshwa kidogo au ikabaki ile ile ya mwaka uliopita kulingana na mahitaji yanayotakiwa iliwekwa tena fomu ya kidato cha kwanza sasa katika kuichukua hiyo fomu naona baadhi ya wazazi walichanganya kwenye fomu ya kujiunga kidato cha tano na fomu ya kujiunga kidato cha kwanza wakajikuta wanalipia shilingi 80,000/= kimakosa”,ameongeza Mwl. Kagunze.
Katika hatua nyingine amewakaribisha wanafunzi wote wa kidato cha kwanza waendelee na masomo huku akibainisha kuwa tangu shule ifunguliwe wanafunzo wote wanaendelea na masomo na hata wanafunzi waliofika bila hiyo pesa walipokelewa na wasio na sare pia wamepokelewa na wanaendelea na masomo.
Aidha amesema mpaka saa tisa alasiri Jumamosi Januari 20,2024 wanafunzi 100 wameripoti shule kati ya wanafunzi 143 waliopangwa kujiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga.
Nao baadhi ya wazazi akiwemo Hellen Andrea Luhamba aliyetumiwa fedha yake kupitia simu yake na Ibrahim Lyanga aliyefika shuleni wamekiri kurudishiwa pesa zao baada ya kuelezwa na uongozi wa shule kwamba hakuna michango kwani elimu ni bure huku Mkuu wa shule hiyo, Nurah Kamuntu akieleza kuwa zoezi la kurejesha fedha kwa wazazi linaendelea vizuri na kila mzazi atapata pesa yake.