Na John Mapepele
Kamati ya Bunge ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika zoezi la kuwahamisha wananchi kwa hiari katika Hifadhi ya Ngorongoro na kuboresha maisha yao katika maeneo yaliyotengwa.
Akizungumza mara baada ya kamati hiyo kukagua utekelezaji wa kazi za ujenzi wa nyumba bora za wananchi wanaohamia kwenye eneo la Msomera leo Januari 10, 2024 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara huku akisisitiza kuwa kazi hiyo ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya watanzania.
"Ndugu zangu naomba niseme mambo matatu, kwanza tumeridhika na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wizara ya Maliasili, pili tutoe wito kwa watanzania kuja kutembelea na kuona kazi nzuri ambayo imezingatia haki na ustawi katika eneo hili, na mwisho natoa wito kwa wananchi waliosalia kwenye Hifadhi ya Ngorongoro waje huku ili nao wapate maisha yaliyoboreka" Amesisitiza Mhe. Mnzava
Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine wanaoshiriki kwenye zoezi hili kuiga mfano wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kukamilisha zoezi hili kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amepongeza Kamati hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kusimamia Serikali huku akimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kwenda kuheshimisha utu wa watanzania kupitia zoezi hili ambalo linalengo la kuboresha maisha yao.
Amesema wizara itaendelea kufanya kazi kwa kizingatia maelekezo ya Serikali katika kutekeleza jukumu hili na kutoa wito kwa wananchi waliosalia hifadhini kuja kujipatia maisha bora.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Alberto Msando amemshukuru Mhe. Rais na Kamati na kusisitiza kuwa kama wilaya wapo tayari kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi.
"Kama wilaya tupo tayari kupokea maelekezo yenu, pia tunaomba mkawe mabalozi wetu kutusemea kwa wananchi malengo mazuri ya mradi huu." Amefafanua Mhe. Mkuu wa Wilaya
Ameongeza kuwa mradi huu unalenga kutoa haki zote za msingi kwa wananchi na kuboresha maisha yao kwa kuwapatia huduma kama kuwajengea shule, hospitali, umeme na barabara.
Mkuu wa Operesheni ya zoezi la ujenzi wa nyumba bora 5000 kwenye eneo la Msomera Kanali Sadiki Mihayo ameeleza kuwa timu yake imejipanga kikamilifu kutekeleza mradi huo kwa wakati kulingana na ratiba.