Watu watatu wa Familia moja Mtaa wa Lukuyu Kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro wamefariki kwa kusombwa na maji wakati wakijaribu kujiokoa baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi pembezoni mwa Mto Mgolole kuzingirwa maji usiku wa kuamkia Januari 10 kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mkoa wa Morogoro limeongoza wananchi katika zoezi la uopoaji wa miili ya watu watatu waliofariki kwa kusombwa na maji ambapo miili miwili tayari imekwisha opolewa akiwemo Asnati Thomas (6) na Theresia Adolfu (73) ambao miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Shababi Marugujo amethibitisha taarifa ya vifo hivyo, amesema wamefanikiwa kuopoa miili miwili na jitihada bado zinafanyika kuopoa mwili wa Mwanahamisi Issa (35) ambaye ni Mama wa Familia ambao haujapatikana.
Katika tukio hilo, Sengo Hamis (47) ambaye ni Baba wa Familia hiyo amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake wakati akijaribu kujiokoa na sasa anaendela na matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Social Plugin