-AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI ZAIDI
NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemtaka Mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 kuongeza kasi na nguvu ya utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wapate maji haraka na kuondokana na adha ya ukosefu wa maji.
Mhandisi Mahundi ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maji jana Januari 23 2024, Urambo Mkoani Tabora ambapo ametembelea mradi wa maji wa miji 28 ikiwemo kijiji cha Ndono ambapo bomba la kupeleka maji Urambo linapojengwa.
Aidha Mhandisi Mahundi amewahakikishia wana Urambo kuwa ifikapo mwezi Oktoba 2025 wananchi wa Urambo watakunywa
Maji safi na salama yatokanayo na mradi huo wa maji wa miji 28 unaotoa maji kutoka ziwa Victoria utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 145.
" Wananchi hawa wa Urambo watanufaika na maji kutoka katika bwawa la Kalemela linalojengwa lenye thamani ya shilingi Bilioni 5 na niwahakikishie mpaka ifikapo mwezi Oktoba changamoto ya maji hautakuwepo eneo hili"amesema Mhandisi Mahundi
Kadhalika Mhandisi Mahundi amewapongeza Mkurugenzi wa TUWASA Eng. Mayunga Kashilimu, Meneja wa RUWASA Mkoa Eng. Hatari Kapufi, Mameneja wa RUWASA Wilaya zote za Tabora na watumishi wote wa Maji Mkoa wa Tabora kwa kazi wanayofanya ya kuhakikisha wanasambaza maji kwa wananchi wa mkoa wa Tabora, kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi na kuwashirikisha wananchi katika huduma ya maji na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yao.
Wakitoa Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo ya maji TUWASA na RUWASA wamemueleza Mhandisi Mahundi kwamba utekelezaji wa mradi kuelekea Urambo eneo la Ndono umesimama kutokana na hali ya mvua na kwamba maeneo mengine ujenzi unaendelea.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Elibariki Bajuta ametumia wasaa huo kuelezea kuhusu kupungua kwa kasi ya ujenzi kwa mkandarasi wa mradi huo kuwa ni pamoja na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini na kwamba mitambo ya ujenzi inazama na tope.
Social Plugin