MKUU WA WILAYA YA KONGWA AAGIZA WALIOJIFELISHA DARASA LA SABA KURUDIA DARASA.

 


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma  Mayeka Simon Mayeka, ameagiza wanafunzi waliofeli mtihani wa darasa la Saba mwaka 2023 kinyume na matarajio kurudia darasa hilo ili kutimiza azma ya Serikali ya Kuifanya elimu ya kidato cha nne kuwa ya lazima. 

Kufuatia hali hiyo  amewaagiza watendaji wa Kata zote Wilayani hapa kuwasaka wanafunzi wote waliojifelisha watafutwe popote walipo ili waweze kurejea shuleni na kuendelea na  masomo ya darasa la saba.

Mayeka ametoa agizo hilo Januari 08, 2024,  Katika ukumbi wa Shule ya Msingi Mkoka wakati akizungumza na wazazi na walezi wa Wahitimu wa Darasa la saba mwaka 2023 waliofeli mitihani kinyume na matarajio yanayotokana na tathmini endelevu iliyofanywa na Divisheni ya elimu ya awali na msingi. 

Amesema  wazazi wanaopaswa kuhakikisha watoto wao wanakwenda shuleni mapema iwezekanavyo ifikapo January 09, 2024 ili kuendelea na masomo ya darasa la saba, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayepuuza agizo hilo.

Amesema ni aibu kupoteza muda kujadili suala la wazazi kuwa kikwazo kwa watoto wao kupata elimu katika ulimwengu wa sasa na ameahidi kuishughulikia changamoto hiyo kikamilifu. 

"Naagiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kuhakikisha wanakwenda shuleni hata kama hawana sare za shule, na wazazi kila mmoja ahakikishe anatoa ushirikiano wakutosha kwa kuwapelekea chakula watoto,naamini siri kubwa ya ufaulu wa mwanafunzi ni kupata chakula awapo shuleni " amesema Mayeka. 

Sambamba na agizo hilo amewahimiza wazazi wote wenye wanafunzi shuleni kushirikiana na walimu kuboresha zoezi la ufundishaji na ujifunzaji kwa kuhakikisha wanafunzi hao wanapata chakula wawapo shuleni kwani inasaidia kuinua kiwango cha Ufaulu. " "Hakuna kitu chochote kinachosaidia ufaulu kwa wanafunzi zaidi ya wanafunzi kupata chakula Shuleni" amesema

Mayeka kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Remidius Mwema ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Manyara, ameahidi pia kulivalia njuga suala la ajira kwa watoto na kueleza kuwa atakula sahani moja na waajiri haramu wa  watoto ikiwemo wale wanaowapa ajira za kazi za ndani katika miji mbalimbali.

"Katika hili natoa wito kwa jamii kushirikiana  kuwafichua madalali wote  wanaojihusisha na kushawishi watoto wenye umri wa kuwa shuleni kwenda kufanya kazi za ndani, hii ni aibu niwambe pia Wataalamu ngazi ya Wilaya, kata na vijiji wakiwemo Walimu kushirikiana na wazazi katika jitihada za  kuondoa changamoto hiyo ya aibu ya kujifelisha kwa wanafunzi, "amesisitiza

Aidha ametumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kuweka utaratibu maalumu wa kuwasaidia wanafunzi wasio na uwezo kwa kuwalipia gharama za masomo katika ngazi mbalimbali za kielimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri  White Zuberi  amepongeza agizo hilo ambalo limetokana na maazimio ya vikao vya kisheria vya Halmashauri na kwamba uamuzi huo unalenga kuwakomboa wanafunzi hao na kwamba wasijihisi unyonge kwa kuwa dhamira ya uamuzi huo wa kuwarejesha shuleni ni kuwakomboa na siyo kuwaumiza. 

Kwa upande wake  Mkuu wa Divisheni ya Elimu Awali na Msingi Mwalimu Margareth Temu amesema jumla ya Wanafunzi 416 wa darasa la saba walifeli mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka Jana (2023) kinyume na matarajio ingawa halmashauri ya  Kongwa inajivunia kupanda ufaulu kwa asilimia 8% ikilinganishwa na matokeo ya mwaka juzi. 

Kati ya idadi hiyo wanafunzi wapatao 74, wanatokea tarafa ya Zoissa, ambapo 53 kati yao walishiriki kikao hicho muhimu. 

Naye Spika mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Kongwa Job  Ndugai amekemea tabia  ya baadhi ya wazazi kuwashawishi watoto wao kujifelisha kwa malengo ya kuajiriwa kazi za ndani na kuwataka kuacha mara Moja  kwani kitendo hicho hakina faida yoyote. 

"Tunapaswa kuwahamasisha watoto kujitambua na kufahamu kwamba maisha yao ya baadaye yanategemea sana elimu, wazazi na walezi wanao wajibu wa kushirikiana na watoto  wao kufanikisha ndoto zao, ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali ili kujikimu katika familia, "amesisitiza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post