Na Dotto Kwilasa,DODOMA
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) Deus Sangu, amesema kuwa Muswada wa Uwekezaji wa Umma unatarajiwa kupelekwa bungeni ili kufanya marekebisho kwenye ofisi ya msajili wa hazina na kuleta ufanisi kwenye masuala ya uwekezaji binafsi.
Hayo yamebainishwa bungeni Jijini Dodoma na Mwenyekiti huyo wa PIC wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha zoezi la kupokea maoni ya wadau kuhusu sheria hiyo kufutwa na kuongeza kuwa endapo Muswada huo utapitishwa utasaidia kuanzisha Taasisi ya Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itachukua majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina .
Amesema lengo la muswada huo ni kufanya marekebisho makubwa kwenye ofisi ya msajili wa hazina ambayo ilikuwa na majukumu ya kusimamia mashirika ya umma 304 japo Mashirika hayo hayajaonesha tija kwenye mapinduzi ya uwekezaji.
Licha ya hayo amesema tangu kuanzishwa kwa ofisi ya msajili wa hazina kumekuwa na ombwe kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma hivyo juhudi zaidi inahitajika ili kuleta tija.
"Serikali imewekeza na kuonesha mfano kwenye maeneo mengi lakini suala la uwekezaji hasa binafsi bado halijatiliwa mkazo inavyohitajika,kuanzishwa kwa mfuko wa uwekezaji kutasaidia kuvutia wawekezaji binafsi ,baada ya mchakato huu sasa tunaingia kwenye hatua ya kuchakata tuje mawazo ya kupeleka bungeni, "amesisitiza
Pamoja na hayo amesema iwapo Bunge litaridhia kupitisha muswada huo Ofisi ya Msajili wa Hazina itafutwa na kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itakuwa na dhima kusimamia kwa ukaribu mashirika ya umma.
Sangu amesema ," Kwa mujibu wa takwimu zilizopo hadi kufikia Juni mwaka jana kulikuwa na mashirika ya umma 304 ingawa tija inayokusudiwa bado imekuwa iko chini,Serikali imewekeza zaidi ya sh.trilioni 76.7 katika mashirika hayo ambapo fedha hizo ni bajeti ya miaka miwili ya nchi, "amesema na kuongeza;
“Lengo la serikali ni kuona uwekezaji unakuwa na tija katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa sababu ndiyo muwekezaji mkubwa,”amesema.
Aidha Mbunge huyo wa Jimbo la Kwela (CCM) amesema baada ya muswada huo kupitishwa utaanzisha Mfuko wa Uwekezaji ambapo itahakikisha mashirika yote yanakuwa na mitaji ya kutosha kwa ajili ya kujiendesha.
Amesema wamepokea maoni ya wadau zaidi ya 50 na tunaendelea kupokea kupitia ofisi ya Bunge baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyachakata na kuwasilisha ndani ya bunge ili kuridhia kuwa sheria kamili ambayo itaanzisha taasisi mpya, "amesema.
Ameongeza kuwa ”Tunaamini sheria hii ikipita kutakuwa na mambo mazuri ikiwemo wakurugenzi wa bodi za taasisi kutewuliwa kwa njia ya ushindani ambapo na wale wenye sifa ndio watapata nafasi.
Social Plugin