Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ARIDHIA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI WA ZIWA VICTORIA KUFIKISHWA WILAYANI USHETU

 



Na Mathias Canal, Ushetu-Kahama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanza kwa utekelezaji wa kufikisha mradi wa maji wa ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ushetu.

Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso ameyasema hayo leo tarehe 9 Januari 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Busenda katika kata ya Chona, wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Waziri Aweso amesema kuwa tayari amefanya mawasiliano na watendaji na tayari tenda ya utekelezaji wa mradi wa maji imeshatangazwa ndani ya siku 30 mkandarasi atakuwa amepatikana na kazi itaanza.

Pia Waziri Aweso amezindua mradi wa maji wa maji Busenda ambao umegharimu kiasi cha Shilingi 344,480,060 ikiwa ni fedha zinazotokana na mpango wa malipo kwa matokeo (PforR) huku akimpongeza Mhandisi wa RUWASA mkoa wa Shinyanga kwa kusimamia kwa weledi mradi huo.

Waziri Aweso amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ni kutokana na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama na ya uhakika katika kijiji cha Busenda.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani amemshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwani mradi huo utasaidia kumtua ndoo mama kichwani na kumuongezea muda wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kupunguza maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Wananchi wapatao 3,551 watanufaika na huduma ya majisafi na salama, Mbunge Cherehani amempongeza Rais Samia kwa kukubali kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maji katika wilaya ya Kahama.

Mhe Cherehani ameitaja changamoto kubwa katika jimbo hilo kuwa ni ukosefu wa maji kwani kata 11 kati ya 20 hazijafikiwa na mradi wa maji hivyo mradi wa maji ya ziwa victoria utakuwa muarobaini wa kadhia hiyo.

Utekelezaji wa mradi wa Maji Busenda umefanywa na wataalamu wa ndani wa RUWASA kwa mfumo wa Force Account ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 10 Machi 2023 na kukamilika tarehe 5 Septemba 2023.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com