Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amefanya ukaguzi wa uandikishaji wa wanafunzi kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari zilizopo manispaa ya Shinyanga ikiwa ni siku ya kwanza kwa wanafunzi kuripoti shuleni.
Zoezi hilo limefanyika leo January 08, 2024 shule ya msingi Mwenge,shule ya sekondari Ngokolo pamoja na shule ya sekondari ya wasichana Shinyanga zilizopo manispaa ya shinyanga.
Akizungumza wakati alipotembelea shule hizo RC Mndeme amewapongeza wazazi na walezi kwa maandalizi mazuri waliofanya na kuwaandikisha watoto kuanza masomo mashuleni huku akiwasisitiza kupeleka watoto shule kwani ni haki ya msingi kila mtoto kupata elimu.
“Ni haki ya msingi kwa kila mtoto kupata elimu, niwaombe wazazi na walezi waandikisheni watoto, tusitumie watoto kama chanzo cha kujipatia utajiri kwa kuwaozesha ili tu wapate mali, wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwaajili ya watoto wawapo shuleni sambamba na utoaji wa elimu bila malipo tumuunge mkono kwa kuhakikisha watoto wetu wanaanza shule na niwahakikishie mkoa wa shinyanga tumejipanga kupokea watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza pamoja na darasa la awali”, amesema RC Mndeme.
Pia RC Mndeme ameahidi kufanya ukarabati wa majengo ya shule ya msingi Mwenge kutokana na ukongwe wa shule hiyo ambapo imeanza kufanya kazi tangu mwaka 1938 mpaka sasa.
Akieleza matarajio ya uandikishaji wa wanafunzi kulingana na sense ya watu na makazi iliofanyika mwaka 2022 afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako amesema kwa elimu ya awali walitarajia kuandikisha wanafunzi elfu 75, 079 huku kidato cha kwanza ikiwa ni kwa mujibu wa wanafunzi waliofaulu ambao ni elfu 38,963 kwa mkoa wa Shinyanga.
“Kama tunavyofahamu kwenye sense kuna kipengele cha umri kulingana na wananfunzi wanaotarajia kwenda shule ambapo kwa elimu ya awali tumetarajia kuandikisha wanafunzi 75,079 lakini mpaka sasa tumeshaandikisha wanafunzi 47,187 sawa na asilimia 62, kwa upande wa darasa la kwanza tumeandikisha wanafunzi 44,332 sawa na asilimia 64 na kwa upande wa kidato cha kwanza ni kwa mujibu wa wale waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza ambapo walifaulu 38,963 tunaendelea kukusanya data za uandikishwaji kwenye shule zote”, amesema Ndalichako.
Aidha zoezi hilo liliambatana na utoaji wa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi waliowasili shuleni ambapo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ameongoza zoezi la ugawaji wa madaftari, karamu kwa wanafunzi.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndemeakigawa zawadi ya vifaa vya kujifunzia kwa wananfunzi wa shule ya msingi Mwenge.
Social Plugin