TAMWA ZNZ YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUONGEZA JUHUDI KUANDIKA HABARI ZA WANAWAKE NA UONGOZ


Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) Dkt. Mzuri Issa amewataka waandishi wa habari vijana kuongeza juhudi katika kuandika habari za wanawake na uongozi ili kuishawishi jamii kuliunga mkono kundi hilo hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Akizungumza katika mkutano uliowashirikisha wadua kutoka shirika la National Endowment for Democracy (NED), waandishi wa habari Vijana, Wakurugenzi wa Redio na Wahariri wa vyombo vya habari, Dkt Mzuri amesema kuna mambo kadhaa yanayowakwaza wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Dk Mzuri amesema TAMWA ZNZ kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali kwa waandishi wa habari hao ili kuwaongezea zaidi ujuzi waweze kuandika habari za wanawake na uongozi, pamoja na kuondosha mitazamo hasi katika jamii.

“Tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu 2025 hivyo waandishi wa habari tunawategemea katika upande huu kuandika zaidi na kufanya vipindi vingi ili tuone kasi ya wanawake inakuwa kubwa katika kugombea ngazi mbalimbali majimboni,” Dk Mzuri.

Nae meneja wa mradi wa kuwawezesha waandishi wa habari vijana (YMF) Africa, Merry Kangunyi amesema wamefarajika na jitihada mbali mbali zinazofanywa na TAMWA ZNZ katika kushawishi jamii kuondokana na mitazamo hasi, hususan wanawake kugombea nafasi za Uongozi.

“Tumefarajika na kazi kubwa inayofanywa na TAMWA ZNZ katika kuongeza nguvu na kuifahamisha jamii kujuwa haki zao pamoja na kugombea nafasi za Uongozi kuanzia katika ngazi ya familia hadi Taifa,” Merry Kagunyi.

Afisa Mradi wa kuwawezesha waandishi vijana kuandika habari za wanawake na uongozi kutoka TAMWA ZNZ Tatu Ali Mtumwa

amesema waandishi wa habari wamekuwa chachu ya maendeleo kwa kuhamasisha usawa wa kijinsia ili kufikia asilimia 50/50 kwa wanawake na wanaume katika ngazi za maamuzi.

Mradi wa kuwawezesha waandishi wa habari vijana (YMF) kuandika habari za wanawake na uongozi uliowashirikisha waandishi vijana ishirini na wanne (24) kutoka Uguja na Pemba ambao unatekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na shirika la National Endowment for Democracy (NED).




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post