Afisa Udhibiti Ubora TBS, Bw. Felix Makarius akitoa elimu kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la TBS katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar kwaajili ya kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
********************
USHIRIKIANO mzuri baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kero za bidhaa ambazo hazina viwango kutoka Zanzibar kwenda Bara.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibari kwa ajili ya kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema shirika hilo limeshiriki maonesho hayo kwa ajili ya kuelimisha na kueleza umma mafanikio ambayo TBS limepata miaka 60 iliyopita, ambapo moja ya mafanikio makubwa ni ushirikiano baina yake na ZBS.
"Ilikuwa ni muhimu kuwa na ushirikiano huu kwa sababu biashara kati ya Visiwani (Zanzibar) na Bara ni kubwa sana na zinahusiana na bidhaa mbalimbali ambazo zinadhibitiwa viwango na TBS na ZBS, kwa hiyo mnaweza kuona umuhimu wa kuwa na ushirikiano huo," alisema Dkt. Ngenya.
Alisema ushirikiano huo umewezesha kupunguza bidhaa ambazo hazina ubora kwa kiasi kikubwa baina ya pande hizo mbili za Muungano.
Dkt. Ngenya alisisitiza kwamba bidhaa baina ya pande hizo mbili zimeongezeka ubora kwa kiasi kikubwa sana.
Kwa upande wake mtaalam wa lishe na Kiongozi wa Jumuiya ya Wenye Viwanda Vidogo Tanzania (WAJATA) , Issa Njoka, alipongeza TBS kwa kuhudumia Watanzania na kuimarisha viwanda kea kuhakikisha vinazalishwa bidhaa bora ambazo zinalinda afya za watumiaji.
Njoka ambaye alitembelea banda la TBS kwenye maonesho hayo, alisema yeye kama mzalishaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo kwa kufika kwenye banda la TBS alipata huduma na maelekezo ya kina kutoka kwa maofisa wa shirika hilo waliokuwa wanatoa elimu kwa wananchi.
"Lakini nimeweza kuelewa kuwa kila Mtazania na wazalishaji kwa ujumla wanatakiwa wafike TBS ili waelimishwe ni namna gani wanaweza kupata bidhaa bora ili pale unapokuwa unakula kitu lazima kiwe kimethibitishwa na TBS," alisema Njoka na kuongeza;
"Ni lazima Watanzani tuwe wazalendo tunapotaka kununua bidhaa, ni lazima kuangalia kama ina alama ya ubora ya TBS ili kuepuka kula bidhaa zenye madhara kiafya ambazo zinaweza kusababisha ukapoteza maisha."
Alisema kwenye vyakula zinapatikana sumukuvu na sumu mbalimbali, hivyo kila Mtanzania ajione ni sehemu ya TBS. "Natoa wito kwa kila Mtanzania kuitumia TBS ili kuweza kuboresha bidhaa zetu kupitia shirika hili,"alisema Njoka.
Njoka aliwataka wazalishaji kuhakikisha wanatengeneza bidhaa bora ili waheshimike, kwani wakiitumia TBS wanaenda kunyanyua taifa kuwa Taifa la viwanda na bidhaa bora.
Afisa Udhibiti Ubora TBS, Bw. Felix Makarius akitoa elimu kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la TBS katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar kwaajili ya kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kaaya (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu katika Mkutano wa Wakuu wa Taasisi wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar.
Social Plugin