Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UGONJWA WA KUHARA NA KUTAPIKA WAUA WATU WATANO KAGONGWA... 18 WABAINIKA KUWA NA KIPINDUPINDU SHY


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza na waandishi wa habari - Picha na MALUNDE 1 BLOG
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amesema watu 18 kati ya 41 ambao walikabiliwa na tatizo la kuhara na kutapika wamebainika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo ambapo mpaka leo Januari 9,2024, wagonjwa 5 pekee wanaendelea na matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo januari 9,2024 Mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme amesema tangu kuanza mlipuko wa ugonjwa huo wa kuhara na kutapika, wagonjwa waliobainika ni 41 na 18 kati yao wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Kipindupindu baada ya vipimo vya kitaalamu kufanyika, ambapo Manispaa ya Kahama wagonjwa 15, Kishapu wagonjwa wawili na Manispaa ya Shinyanga mgonjwa mmoja.

Amesema ugonjwa wa kuhara na kutapika umesababisha vifo vya watu 5 katika kata ya Kagongwa halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga tangu ugonjwa huo ulipozuka mnamo tarehe 28 Desemba mwaka 2023 katika kata hiyo.

“Jumla ya vifo vitano vimetoka kwenye jamii na kifo kimoja kimetokea kwenye zahanati binafsi na wote hawa hawakufanyiwa vipimo vya kuthibitika wamekufa na ugonjwa gani hivyo Vifo vya watu hao watano haikubainika moja kwa moja kwamba walikufa kwa kipindupindu,amesema Mndeme.

Mndeme amesema wagonjwa walioruhusiwa kutoka hospitali mpaka sasa ni wagonjwa 30, ambapo wagonjwa 28 kutoka Manispaa ya Kahama,Kishapu mgonjwa mmoja na Shinyanga manispaa mgonjwa mmoja.

Amesema tayari serikali imetenga vituo vitatu vya matibabu ya ugonjwa huo kikiwemo kituo cha afya Ihapa, Kagongwa na kituo cha afya Kishapu kilichopo wilayani Kishapu.

Aidha serikali ya mkoa wa Shinyanga imesema kuhara na kutapika ni ugonjwa unatokana na kula kinyesi kibichi hivyo wananchi wote wa mkoa huo wametakiwa kuchemsha maji ya kunywa, kutokula vyakula vilivyopoa, kunawa maji tiririka sambamba na matumizi sahihi ya vyoo na kufuata huduma zote za afya.

"Natoa tahadhari kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa ili kukabiliana na ugonjwa huowanatakiwa waepuke kutumia maji yasiyochemshwa, kula matunda bila kuyaosha, kula chakula baridi, matumizi hafifu ya vyoo na kutofanya usafi wa mazingira muda wote",amesema Mndeme.

Mratibu wa ufuatiliaji na udhibiti wa magojwa ya kuambukiza Bw. Mussa Makungu amesema wamewaelekeza Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo,kufanya kaguzi kwenye maeneo yote ya biashara ikiwemo vilabu vya pombe,mama/baba lishe na kwamba zoezi linaendelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com