UMAHIRI WA MAABARA ZA TBS KUFUNGUA MILANGO YA BIASHARA



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TAASISI ya Ithibati ya Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCAS) imethibitisha na kuzipatia vyeti vya umahiri maabara 8 za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua inayopelekea majibu ya maabara hizo kuendelea kukubalika popote duniani jambo linaongeza chachu katika uwezeshaji biashara ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24,2024 Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ithibati ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADCAS) Bi Eva Christine Gadzikwa amesema maabara hizo nane zitaendelea kusaidia na kurahisisha biashara kwani majibu ya maabara hizo yataweza kukubalika na kutumika popote duniani.

"Hakuna haja tena ya kupima bidhaa zilizoidhinishwa hapa Tanzania zitakaposafirishwa nje ya nchi ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa muda na kulinda wateja". Amesema Bi. Gadzikwa.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. David Ndibalema amesema kuwa wanafuraha kubwa ya kupokea vyeti vya umahiri ambapo itasaidia kutambulika kimataifa kwa huduma zinazotolewa na shirika hilo, itasaidia bidhaa zinazozalishwa nchini kuingia katika ushindani kwenye masoko ya nje na ndani ya nchi.

"Kama wote tunavyotambua Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mahusiano yetu yamejikita katika biashara, lakini pia sisi ni wanachama kwenye Jumuiya ya Kusini mwa Afrika, lakini pia mwanachama wa Afrika, ambapo kwenye ngazi ya Afrika tuna soko huru la Biashara. Kutambulika au kupata vyeti vya umahiri ni hatua mojawapo ya kurahisisha bidhaa zetu kushindana katika masoko hayo". Amesema Bw. Ndibalema

Naye Mkurugenzi wa Upimaji na Ugezi wa (TBS) Bw.Ridhiwani Matange ameeleza kuwa kupata vyeti vya umahiri ni jambo kubwa la kujivunia kwani mchakato wa kupata vyeti hivyo inahitaji uwekezaji wa rasimali watu na vifaa vya kisasa na TBS imewekeza kwenye mahitaji hayo.

Shirika la Viwango limepata vyeti vya umahiri kwa maabara zake zote 8.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ithibati ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADCAS) Bi Eva Christine Gadzikwa akifungua hafla ya upokeaji vyeti vya umahiri wa maabara leo Januari 24, 2024 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. David Ndibalema akizungumza katika hafla ya upokeaji vyeti vya umahiri wa maabara za TBS leo Januari 24, 2024 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ugenzi wa (TBS) Bw.Ridhiwan Matenge akizungumza katika hafla ya upokeaji vyeti vya umahiri wa maabara za TBS leo Januari 24, 2024 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau pamoja na watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania wakiwa katika hafla ya upokeaji vyeti vya umahiri wa maabara za TBS leo Januari 24, 2024 katika Ofisi za TBS Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post