Taasisi za Wakala wa vipimo za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (WMA) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZAWEMA) zimetiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) ili kuimarisha utendaji kazi wao katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubadilishana utaalamu na vitendea kazi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi wanao hudumiwa kwa upande wa Bara na Visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini huo katika Ukumbi wa Dokt Mwinyi kituo cha maonesho ya biashara Nyamanzi Fumba Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Hashil Abdallah amesema ni vyema kuimarisha mashirikiano kati ya taasisi hizo ili kuhakikisha vipimo vyote vinakuwa sahihi na mnunuzi wa bidhaa anapata kulingana na thamani ya fedha anayotoa.
Dkt. Hashil amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Wakala wa Vipimo ndio taasisi pekee inayopaswa kusimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha kuwa vipimo vinavyotumika katika biashara viko sahihi, na kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili kuepusha madhara yatokanayo na vipimo batili na kulinda walaji na watumiaji.
Aidha, amesema makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi utakaopelekea kufikia malengo ya Taasisi hizo kwakuwa taasisi ya Wakala wa Vipimo Bara (WMA) ilianzishwa muda mrefu na inauzoefu wa muda mrefu na vifaa vingi vya kisasa kwa mashirikiano haya itaiwezesha zaidi taasisi ya ZAWEMA kutumia pia vifaa hivyo na wataalamu ili kusimamia matumizi sahihi ya vipimo katika sekta nyingi zaidi.
Kadhalika, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Ndugu. Ali Khamis Juma ameeleza kuwa mashirikiano baina ya taasisi za WMA na ZAWEMA ni mashirikiano ya kudumu kwa muda mrefu sio ya kipindi cha muda mfupi kwani hivyo itaiwezesha taasisi ya ZAWEMA kukua zaidi na kuingia katika maeneo mengi ya kiutendaji kama ilivyo upande wa WMA Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bara (WMA) Bi. Stella Kahwa ameeleza kuwa mashirikiano baina ya WMA na ZAWEMA yamekuwepo kwa muda japo hayakuwa rasmi kimaandishi na sasa yamekuwa rasmi taasisi hizi zitazidi kuimarisha zaidi mashirikiano hayo na mara nyingi WMA na ZAWEMA hushirikiana hata katika kuendesha kaguzi mbalimbali visiwani Zanzibar kwa wauzaji wa vito na madini, mafuta na hata katika sekta ya gesi ili kuhakikisha vipimo vinakuwa sahihi wateja hawapunjiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Bw. Mohammed Simai Mwalim ameeleza kuwa endapo vipimo vitasimamiwa kwa usahihi katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi itasaidia Serikali kukusanya kodi kwa usahihi.
Hata hivyo alisema endapo vipimo hivyo havitasimamiwa vyema itasababisha wananchi kupata huduma au bidhaa ambazo haziendani na thamani ya fedha wanayotumia.
Mkurugenzi Mohammed ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa Tanzania bara na Zanzibar kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na endapo watakutana na changamoto yoyote inayohusu vipimo wafike kwenye ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kupata msaada wa kitaalamu.
Hata hivyo aliwaonya Wamiliki wa vipimo kutochezea vipimo kwa lengo la kuwaibia wananchi, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo ambavyo vinakatazwa hata kwenye maandiko matakatifu.
Nao Washiriki walioshuhudia utiaji wa saini huo walisema kuwa makubaliano hayo yametiwa saini katika kipindi muafaka cha kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na yataongeza mashirikiano zaidi ili kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi hayo.
Hati hiyo ya makubaliano ya kiutendaji yalisainiwa na Mtendaji Mkuu wakala wa vipimo Bara (WMA) Stela Kahwa na kwa upande wa Zanzibar Mkurugenzi wakala wa vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Mwalim Simai.