Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MVIWATA WAZINDUA MRADI WA BARIDI SOKONI


 Mkurugenzi wa MWIWATA Steve Ruvuga akizungumzia mradi huo mbele ya washiriki wa uzinduzi huo iliyofanyika mkoani Morogoro.
Na Christina Cosmas, Morogoro

MTANDAO wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) umezindua mradi wa Baridi sokoni utakaowanufaisha wakulima 20,000 wa mazao ya malimbichi katika kuongeza uzalishaji na tija, kupunguza upotevu na uharibifu wa mazao shambani na kuboresha lishe kwa familia.

Mkurugenzi wa MVIWATA Steven Ruvuga amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa Baridi Sokoni unaogharimu zaidi ya dola za kimarekani Milioni 5.6 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 11 za kitanzania uliofadhiliwa na Mpango wa kimataifa wa kilimo na usalama wa chakula (GAFSP) na kusimamiwa na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao utatatekelezwa kwa miaka mitano katika mikoa minne nchini.

Amebainisha kuwa, wakulima wadogo wapata 20,000 wanatarajia kunufaika kupitia vikundi, mitandao yao na vyombo vya kifedha, vyama vya ushirika na miradi ya kibiashara vijijini inayomilikiwa na vikundi vya wakulima wadogo.

Ruvuga amesema mradi wa Baridi sokoni unajumlisha miradi miwili pacha ukiwemo utakaojulikana kama Baridi sokoni 1- ulioidhinishwa kwa ufadhili mwaka 2021 na wa pili ni Baridi sokoni 2 ulioidhinishwa kwa ufadhili mwaka 2023 ambao ni mjazilizo wa mradi wa kwanza na ni matokeo ya mchakato wa ushindani miongoni mwa wakulima kutoka Afrika, Asia na Marekani kusini.


Aidha ameeleza kuwa, MVIWATA imejipanga kuchangia katika bajeti hiyo kiasi cha dola za kimarekani 250,000 kama mchango wake katika mradi huo ambao utahusisha mazao ya Malimbichi ikiwemo viazi, nyanya, maharage, njegere, vitunguu saumu, karafuu, mdalasini, pilipili manga na Tangawizi.


Naye Mwakilishi kutoka (AfDB) Salum Ramadhani amesema mradi huo utasaidia wakulima kuendesha kilimo cha Malimbichi vizuri licha ya kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na Covid-19.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com