Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE LONDO AKABIDHI GARI LA WAGONJWA KITUO CHA AFYA MALOLO... ATAKA WASILITUMIE VIBAYA

 

Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Lazaro Londo (kushoto) akikabidhi funguo kwa Daktari kiongozi wa kituo Cha Afya Malolo Yohana Nshashi mara baada ya kuwapatia gari la wagonjwa ili kuwasaidia kwa usafiri na kuwaepusha na vifo visivyotarajiwa.


Na Christina Cosmas, Morogoro



MBUNGE wa Jimbo la Mikumi Wilayani Kilosa mkoani hapa Denis Lazaro Londo amewaasa wakazi wa kata na vijiji vinavyozunguka kata ya Malolo kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa ikiwemo kwenda na gari la wagonjwa walilopata kwenye mambo ya starehe za dunia na kubebea mikaa na kuacha wagonjwa wakifikwa na vifo visivyo vya lazima.



Londo alisema hayo jana wakati akikabidhi gari la wagonjwa katika kata ya Malolo Wilayani Kilosa mkoani hapa ambapo alisema wapo watu ambao wakati mwingine wanakosa uelewa na kuamua kubadilisha matumizi ya mali za Umma kwa manufaa yao binafsi jambo ambalo litaondoa maana ya uwepo wa gari hilo.

 

Aidha Londo aliwataka watumishi wa afya kuwa na ushirikiano thabiti utakaohakikisha wagonjwa wanatumia vyema gari hilo na kuwaepusha na vifo visivyo vya lazima kwa kufika wenye hospitali zilizokusudiwa kwa wakati.



"Sitegemei tena kusikia kuna mtu amefariki kwa sababu ya kukosa usafiri wa kumpeleka kwenye matibabu, gari ndio hilo na mlitunze, lisitumike kubebea mabebi wa watu wala mikaa, watakaobainika nitashughulika nao" alisema Londo.

 

Akipokeà gari hilo Daktari kiongozi wa kituo cha Afya Malolo Yohana Nshashi aliishukuru Serikali ya awamu ya sita na Mbunge Londo kwa kuwapatia gari la wagonjwa ambapo alisema litawapunguzia wagonjwa adha ya kutembea kilometa zaidi ya 100 kupata huduma katika hospitali ya Mikumi.

 

Alisema kituo cha afya Malolo kinahudumia wakazi 13,319 wakitokea kwenye vijiji vinne ikiwemo Malolo B, Malolo A, Mgogozi na Chabi sambamba na kuhudumia vijiji jirani vinavyopakana na Kilosa ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

 

Naye mmoja wa kinamama na mkazi wa Kijiji cha Malolo B Bertha Ngalela aliishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la wagonjwa ambalo litawasaidia kuwafikisha kupata huduma hasa za upasuaji katika hospitali zilizopo Mikumi, Morogoro mjini, Dar es salaam na Iringa ambako ndiko hupata huduma wanaposhindwa kujisaidia katika kituo hicho.

 

“Kutoka hapa hadi barabarani Ruaha Mbuyuni ni Kilometa 8 na ukitoka pale usafiri wenyewe gari ni za kuvizia, labda upandishwe kwenye lori au labda uhangaike tu kutwa nzima palepale bila kupata gari na pengine kuishia kufariki bila kufika Iringa wala Mikumi, lakini kwa kuletewa hili gari tunaamini tutafika hospitali salama na kupona” alisema Ngalela.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com