Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia : EDWARD LOWASSA AFARIKI DUNIA


Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowassa (71) amefariki dunia leo Jumamosi Februari 10,2024  wakati akiendelea kupatiwa  matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)  jijini Dar es Salaam.

Tangazo la kifo cha Lowassa kimetangazwa Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango.

Katika tangazo fupi alilolitoa kupitia televisheni ya taifa TBC, Mpango amesema kuwa Lowassa  ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mwaka 2005-2008 amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Kufuatia kifo cha Lowassa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter ameandika ujumbe ufuatao


"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu. Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito. Katika mawasiliano yangu na familia, nimewaeleza kuwa kama taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21. Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina"


Lowassa alizaliwa Agosti 26,1953.

Lowassa alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania chini ya Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa miaka mitatu, toka 2005 mpaka 2008 alipolazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.

Mwaka 2015 Lowassa alikihama chama tawala cha CCM baada ya kukosa tiketi ya kuwania urais kupitia chama hicho.

Alitimkia chama kikuu cha upinzani cha Chadema ambapo aliungwa mkono kugombea urais na vyama vilivyounda umoja wa upinzani wa UKAWA kwa wakati huo.

Lowassa hata hivyo alishindwa katika uchaguzi huo na aliyekuwa mgombea wa CCM John Pombe Magufuli. Lowassa alirejea CCM mwaka 2019. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com