Na Christina Cosmas, Morogoro
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga amewashauri viongozi vijana kutambua kuwa wana mambo mengi ya kujifunza na kuiga kutoka kwa Hayati Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa aliyosimamia ili kuleta maendeleo nchini.
Mwenyekiti huyo alisema hayo jana wakati akiongea na vyombo vya Habari ambapo alisema Hayati Lowassa alikuwa kiongozi makini, jasiri, shupavu, asiyeogopa kutoa maamuzi yenye maslahi kwa Taifa, huku akiwa mahiri na mwenye uthubutu mwenye kariba za uongozi ambazo vijana wanapaswa kuwa nazo.
Alisema hayati Lowassa aliweza kusimamia na kufuatilia mambo mengi ambayo yalileta matokeo mazuri nchini ikiwemo kampuni ya City water iliyopewa kazi ya kutengeneza miundombinu ya maji jijini Dar es salaam na kuonesha kutowajibika kwa kiwango kikubwa huku ikiwa na uwezo mdogo naye akiwa Waziri wa Maji alitoa maamuzi ya kuvunjiwa mkataba wao.
Aidha alisema Hayati Lowassa aliweza kusimamia kwa ukamilifu katika kila nyanja aliyotakiwa kusimamia na kufuatilia ambapo akitoa maelekezo alihakikisha hayaishii njiani na hivyo wataendelea kukumbuka mchango wake.
Pia alisema akiwa Waziri wa ardhi Lowassa alifanikisha kurejesha eneo la mnazi mmoja baada ya kuwafukuza wavamizi wakitaka kujenga bila kufuata taratibu za sheria za ardhi.
Mhandisi Masunga alisema pia hayati Lowassa alisimamia na kufuatilia na kuleta matokeo mazuri kwenye mgogoro uliokuwepo kati ya mataifa ya Misri walioona wana mamlaka zaidi ya kutumia maji ya ziwa Victoria kuliko watanzania kwa kutumia mikataba iliyosainiwa enzi za ukoloni.
“Kuhusu ziwa Victoria Lowassa akiwa Waziri wa maji alisema hapana haya maji tumepewa na Mwenyezi Mungu yanatoka kwetu, na mito inayoingiza maji humo inatoka kwetu, sasa hatuwezi tukasimamia kwenye mkataba wa kikoloni tukiwa nchi huru, na yale hayakuwa mawazo yetu, tunayahitaji haya maji, na sasa miradi ya maji inaendelea kutoa maji ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na mpango wa Serikali ni kusambaza hadi Tabora na maeneo mengine ya kati ya nchi hivyo alionesha uthubutu wa kutenda” alisema Mwenyekiti Masunga.
Mhandisi Masunga alisema Hayati Lowassa aliweza kusimamia suala la Elimu nchini na kuhakikisha shule za Sekondari za kata zinaanza kujengwa kwa kasi jambo lililosaidia kwa sasa wanafunzi wote wanaendelea na elimu ya Sekondari nchini.