Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la kujenga Taifa kupitia SUMA JKT kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika ujenzi wa nyumba 5000 uliogawanyika maeneo matatu tofauti Wilayani Handeni Msomera na Kilindi Saunyi mkoani Tanga pamoja na Simanjiro Kitwayi B.
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yao ya kikazi katika kijiji cha Msomera ,mwenyekiti wa wakurugenzi wa bodi wa Mamlaka hiyo ,Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amesema kazi kubwa inayofanywa na jeshi katika ujenzi huo ni lazima iungwe mkono na wadau wengine wa kisekta ili kukamilisha zoezi hilo haraka.
Amesema katika ziara hiyo amejionea kusuasua kwa baadhi ya sekta katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo kushauri kila mdau ni muhimu kuhakikisha anatekeleza majukumu yake.
“Suma Jkt mnafanya kazi kubwa ni muhimu sana kila mmoja wetu atimize wajibu wake ili tuimarishe miundo mbinu ya kijiji hiki hasa nyumba ili wananchi waweze kuhamia kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro,”amesema mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Kamishina wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Richard Kiiza amesema hamasa ya wananchi kuhamia katika kijiji hicho ni kubwa ambapo mamlaka itaendelea kuwahamisha kadri wanavyojiandikisha
Kaimu Operesheni Kamanda wa mradi huo Luteni kanali Edward Mwanga amewahakikishia wakurugenzi hao wa bodi kuwa ujenzi wa nyumba hizo utakamilika kutokana na kasi na ari ambayo wanayo katika utekelezaji.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Handeni mheshimiwa Albert Msando amesema wataendelea kuwapokea wananchi wanaotoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora.