Mzee wa miaka 70 amekamatwa kwa mauaji ya kutisha ya mtoto wake wa miaka 32 kufuatia mzozo katika Kaunti Ndogo ya Kianyaga nchini Kenya.
Francis Njagi wa kijiji cha Gwama Kata ya Karumandi anadaiwa kumuua mwanawe James Mwobe baada ya kutofautiana kuhusu matumizi ya kipande cha ardhi. Ripoti ya Citizen Digital ilifichua kuwa kamanda wa polisi wa Gichugu Johnson Wachira alisema Njagi yuko chini ya ulinzi wa polisi na anazuiliwa katika Kituo cha Kianyaga.
Mkewe Njagi, Irene Njagi, alifichua kuwa Mwobe alitaka kupanda Macadamia kwenye kipande cha ardhi, jambo ambalo babake alipinga. Irene alisema mabishano kati yao yalizidi ndipo Njagi alipomchoma kisu mtoto wake na kumuacha akiwa amejeruhiwa huku akivuja damu. Vilio vya Irene na kuomba msaada vilimvutia jirani yake aliyemkimbiza Mwobe katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kianyaga.
Hata hivyo, madaktari walimtangaza kuwa amefariki baada ya kufika katika kituo cha afya. Mwili wa Mwobe ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Kerugoya huku uchunguzi ukiendelea kuhusu kisa hicho cha kusikitisha.
Social Plugin