Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TOSCI YATOA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA KUELIMISHA WAKULIMA MATUMIZI YA MBEGU BORA ZA KILIMO

 




Na Marco Maduhu,SHINYANGA

TAASISI ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imetoa mafunzo kwa Waandishi wa habari mkoani Shinyanga,juu ya kufahamu majukumu ya Taasisi hiyo,pamoja na kutumia Kalamu zao kuelimisha Wakulima umuhimu wa Matumizi ya Mbegu bora za Kilimo.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika leo Februari 24,2024 na kushirikisha baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga, kwa kuwajengea uelewa juu ya Matumizi ya Mbegu bora za Kilimo.

Akizungumza kwenye Mafunzo hayo Mwezeshaji Zera Mwankemwa kutoka TOSCI Makao Makuu, amesema Waandishi wa Habari ni watu muhimu katika kutoa elimu kwa Wakulima kupitia Kalamu zao juu ya Matumizi ya Mbegu Bora za Kilimo na hatimaye kupata Mavuno mengi na kuinuka kiuchumi na Taifa kwa ujumla.
“Waandishi wa Habari kaelimisheni Wakulima kupitia Kalamu zenu na vipindi mbalimbali vya Radio, juu ya umuhimu wa kutumia Mbegu Bora za Kilimo ambazo zimethibitishwa na TOSCI ili wapate Mavuno mengi ya Mazao,”amesema Mwankemwa.

Aidha, ametolea Mfano Mkulima akinunua Mbegu za Mahindi zenye ubora zilizothibitishwa na TOSCI Kilo Moja au Mbili ambapo Hekali Moja atatumia Mifuko Minne au Nane, na akija kuvuna mazao yake atapata Magunia ya Mahindi 13 hadi 15, tofauti akitumia Mbegu zisizo na ubora ambapo atapa Magunia Mawili au Matatu.
Naye Afisa Mkaguzi kutoka TOSCI Joseph Pagu,amewasihi Wakulima pindi wanapokwenda kununua Mbegu ili kuepuka kununua Mbegu Feki, kwamba kwenye Lebo ya TOSCI wakwangue kama Vocha ambapo watakutana na namba, kisha waingize namba hizo na watapata majibu kwamba mbegu hizo zimethibitishwa na TOSCI.

“Ili kujua Mbegu hizo zimethibitishwa na TOSCI Wakulima watabonyeza *148*52* wataingiza namba ambapo zipo kwenye Lebo ya TOSCI mara baada ya kuzikwangua kama Vocha kisha wanaweka Reli na kubonyesha Ok na watapata Majibu hapo hapo,”amesema Pagu.
Amewasihi pia Wakulima kwamba kila msimu wa Kilimo unapofika ni vyema wakawa wananunua Mbegu za Kilimo, na siyo kutumia Mbegu ambazo wamebakisha kwenye Mavuno kuzipanda tena, kwamba hazitawapatia Mavuno mengi hasa zile Mbegu Chotara.

Nao Waandishi wa Habari ambao wamepata Mafunzo hayo, wameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapata elimu ya Matumizi ya Mbegu bora za Kilimo, ambayo wataitumia kuelimisha Wakulima kupitia vyombo vya habari.

Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
Picha ya Pamoja ikipigwa.
Picha ya Pamoja ikipigwa mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.

Chanzo _ Shinyanga Press Club blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com