*Kimeanza uzalishaji, kimetoa ajira kwa watanzania
Na MWANDISHI WETU, MOROGORO
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu, Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Taufiq, amesema wajumbe wa kamati hiyo wamefurahishwa na kukamilika kwa kiwanda cha uzalishaji sukari cha Mkulazi, kilichopo Mkoani Morogoro.
Amesema hayo tarehe 3 Februari, 2023 wakati walipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho na kukuta kimeshaanza uzalishaji sukari.
Mhe. Fatma amesema tayari kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa sukari ambapo kimeanza kuzalisha tani 320 marajio ni kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka, ambapo wamemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu ujenzi wa kiwanda kuendelea, ikimbukwe ya kuwa kiwanda kilianza kujengwa mwaka 2016 chini ya ubia baina ya NSSF na Jeshi la Magereza Tanzania Bara.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema kiwanda hicho kina faida kubwa kwa Taifa ikiwemo kuzalisha ajira kwa wananchi, uzalishaji wa umeme zaidi ya megawati 15 ambapo megawati 7 zinaenda kuingia katika gridi ya Taifa kwa maana kiwanda kitauza umeme huo.
"Tunamshukuru Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanyia kazi changamoto ya sukari kupitia mradi huu ambao unaenda kupunguza tatizo la sukari,"amesema Mhe. Katambi.
Mhe. Katambi alisema wizara inafurahishwa sana na uwekezaji uliofanyika hapa, na pia tunapenda kuona miradi kama hii inayogusa wananchi na watanzania wote inakuwa mingi. Mradi ndio umeanza una faida zaidi ya Billioni 7 na umezalisha ajira za kutosha. (Miradi kama hii ndio Mhe. Rais anataka na ndio itakayotufanya tuwe wa tofauti) aliongezea Mhe. Katambi
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema mradi huo una milikiwa kwa ubia baina ya NSSF na Jeshi la Magereza ambapo NSSF inamiliki asilimia 96 na Jeshi la Magereza asilimia 4.
"Kwetu sisi NSSF ni faraja kubwa kufikia hatua hii kwa sababu ndio lengo la Mfuko kuwekeza katika kiwanda hiki ambapo tunaamini pasipo shaka kitarudisha fedha zilizowekezwa," amesema Mshomba.
Aidha, Bw. Masha Mshomba amewashukuru Kamati ya Bunge kwa ushauri wao wa mara kwa mara.
Vilevile Bwana Mshomba ameshukuru wizara na viongozi wa wizara kwa uongozi wao na ushauri wa mara kwa mara, kwakweli msaada kutoka wizarani na viongozi wa serikalini pamoja na kamati umetusaidia sana kuona ya kwamba tunafika mahala pazuri na kiwanda kimeanza uzalishaji. Aliongeza Bw. Masha
Tayari ripoti kutoka kwa wataalamu zinaonyesha ya kwamba uwekezaji wote huu utakuwa umesharejeshwa katika kipindi kisichozidi miaka minne na nusu, huu ni mradi mkubwa sana na wenye manufaa makubwa sana kwa watu wote yaani wananchi kwa ujumla na serikali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea mradi huo na kutoa ushirikiano wa kuboresha mradi huo.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Majungu Liro, amesema Jeshi la Magereza ni mojawapo ya wabia katika mradi huo mkubwa, ambao umeweza kuongeza ajira kwa wananchi. Pamoja na kwamba sisi ni wabia katika mradi huu, sisi ndio tunahusika na ulinzi wa kiwanda hiki kwa asilimia 100. “Jeshi la Magereza ni wabia hapa lakini sisi tunahusika na ulinzi wa kiwanda hiki kwa asilimia 100” Alisema Kamishna Msaidizi Liro.
Nao baadhi ya wajumbe wa kamati Mhe. Boniphace Getere, Almas Maige na Neema Lugangira wameipongeza serikali kwa kazi kubwa iliyofanyika hapa na wamefurahi kuona kiwanda kimeanza uzalishaji sukari. Aidha wamempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa kuendeleza miradi kama hii.
Selestine Some, Mtendaji Mkuu wa Mkulazi, amesema ujenzi wa kiwanda hicho ulianza Julai 2016 na ilipofika tarehe 28 Novemba 2023 walianza uzalishaji wa sukari kwa majaribio.
Amesema kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka. Amesema mpaka sasa mradi umetoa ajira kwa wananchi 2020 ambazo ni ajira za moja kwa moja huku zaidi ya watu 8000 wakinufaika na mradi huo.
Tags:
habari