Imeelezwa kuwa Tohara kinga ya hiari kwa wanaume imechangia kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Mkoani Shinyanga kupitia Afua ya Tohara kwa wanaume inayotekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wa Afya Hatua kwa kshirikiana na AFYA PLUS pamoja na Serikali kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The U.S. Center for Disease Control -CDC)
Kwa kipindi cha Januari 2022 hadi Desemba 2023, Afua ya tohara kwa wanaume kupitia mradi wa Afya Hatua uliwafikia kwa huduma za tohara kinga jumla ya wanaume 73,927 wenye umri wa miaka 15 na zaidi kupitia kliniki za tohara 35 zinazotoa huduma za tohara na huduma mkoba zilizofanyika katika vituo 145 vya kutolea huduma za afya mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 19,2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa tatu wa mradi (2023/2024), mradi huo ulifikia jumla ya wanaume 26, 752 wenye umri wa miaka 15 na zaidi, hii ikiwa ni asilimia 29% ya lengo la mwaka huo wa fedha ambalo ni kuwafikia wanaume 91,022.
“Tumevuka lengo kwa sababu robo tunatakiwa tutoe kwa asilimia 25 lakini sisi tumefikia asilimia 29. Lakini hata kwa miaka ya nyuma pia tumekuwa tukifanya vizuri na hii ni kwa sababu ya ushirikishwaji na ushirikiano unaopatikana katika ngazi ya mkoa, halmashauri na ngazi za jamii”,amesema Dkt. Ndungile.
“Tumeona mafanikio makubwa ya Mradi huu wa Tohara kwa wanaume ulioanza kutekelezwa Mkoani Shinyanga Oktoba mwaka 2021 lengo hasa la mradi huu ni kama sehemu mojawapo ya mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na THPS kwenye eneo la kuzuia Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hasa kwa watu wazima hasa wanaume kwa kutoa huduma ya tohara ili kupunguza maambukizi Mapya ya VVU”,ameongeza Dkt. Ndungile.
Amebainisha kuwa, hivi sasa mwitikio wa wanaume kupata huduma ya tohara ni mkubwa sana, ndiyo maana hata malengo wameanza kuyafikia na hata kuvuka malengo hivyo kutoa wito waendelee kuitikia, waendelee kupata huduma ya tohara kwenye maeneo yao na kwenye vituo ambavyo vimeainishwa kwa ajili ya kupata huduma ya tohara.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile.
“Kwa sasa mwitikio wa wananchi ni mkubwa sana tofauti na mwanzo, watu labda walikuwa wanaogopa kwamba tohara itapunguza nguvu za kiume, itabadilisha labda maumbile kwa hiyo kulikuwa na hiyo hofu. Hivi sasa watu wameona kwamba hakuna madhara, zaidi ni kwamba wanaepushwa na maambukizi ya VVU na hata magonjwa mengine kama haya ya via vya uzazi au magonjwa ya ngono”,amesema.
Amefafanua ,kuwa huduma ya utoaji wa huduma za tohara, inaambatana na huduma zingine za afya ambazo pia zinakuwa msingi mkubwa katika kuhakikisha kwamba maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI yanapungua ambazo ni pamoja na elimu kwa wanaume wanaofika kupata huduma za tohara hupatiwa huduma ya Upimaji wa VVU na wale wanaogundulika kuwa na maambukizi hupewa rufaa ya kwenda kuunganishwa na huduma ya Tiba na Matunzo.
“Lakini pia tunaendelea kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwani hili ni tatizo kubwa lililopo katika mkoa wa Shinyanga na namna gani ya kuepuka masuala hayo lakini pia tunatoa elimu ya magonjwa ya zinaa/ magonjwa ya via vya uzazi”.
“Huduma hii ya tohara inayotekelezwa kwenye vituo 35 vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa wa Shinyanga, huduma mkoba 145 ilitupa fursa nzuri ya kutoa chanjo ya UVIKO 19 kwa kundi la wanaume, hii ilitupa fursa nzuri kufanya vizuri kimkoa na hata kufikia malengo ya utoaji chanjo ngazi ya mkoa”,amesema Dkt. Ndungile.
Mganga huyo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wadau kuendelea kufanya kazi na kutoa huduma zinazoendelea kutolewa kwa wananchi.
Dkt. Peter Mlacha
Kwa upande wake, Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha amesema tohara Kinga imesaidia kupunguza maambukizi ya VVU kwa wanaume kutokana na wanaume kuhamasika kupata tohara kinga kwa hiari baada ya kupata elimu ya tohara na kuachana na imani potovu kuhusu tohara.
Naye Mratibu wa Huduma za Tohara kutoka Shirika la AFYA PLUS, Dkt. Challo Charido amesema tohara kinga inampunguzia mwanaume kupata maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia 60, kuimarisha usafi, kujikinga na magonjwa ya zinaa na saratani ya uume na mlango wa shingo ya uzazi kwa wanawake hivyo kuwasihi wanaume kufanyiwa tohara.
Ameeleza kuwa AFYA Plus kwa kushirikiana na THPS na Timu ya Usimamizi wa Afya ya Mkoa/Halmashauri inaunga mkono utoaji wa huduma za tohara kinga kwa wanaume.
Mratibu wa Huduma za Tohara kutoka Shirika la Afya Plus, Dkt. Challo Charido akielezea faida za kufanya Tohara Kinga kwa wanaume
Amezitaja mbinu wanazotumia katika utoaji wa huduma za tohara kuwa ni huduma za kila siku za tohara kinga kwa wanaume inayotekelezwa katika vituo 35 vya afya ambapo watoa huduma waliopatiwa mafunzo ya tohara kinga kwa wanaume hupangiwa majukumu katika kliniki ya tohara ya wanaume na kituo kinachosimamia utoaji wa huduma za kawaida kwa wanaume wenye umri kati ya miaka 15 na zaidi.
"Mbinu nyingine ni utoaji wa huduma mkoba za tohara kinga inayolenga kufikisha huduma katika maeneo ya mbali na ambayo ni magumu kufikika. Kupitia huduma hizo watoa huduma kutoka kliniki ya tohara ya hospitali kwa kushirikiana na watoa huduma wengine wa afya, wahamasishaji wa jamii, na viongozi wa jamii huainisha maeneo yaliyo na uhitaji mkubwa wa huduma hii",amesema Dkt. Charido.
“Kupitia uhamasishaji wa jamii unaofanywa na wahamasishaji wa kujitolea wa jamii, wanaume ambao hawajatahiriwa hutambuliwa na kuletwa kwenye huduma kwa msaada wa wahamasishaji jamii wa kujitolea, watoa huduma za afya, au viongozi wa jamii. Uratibu wa huduma za tohara kinga hufanywa na kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu kwa kuzingatia idadi ya wanaume walioainishwa kwa ajili ya kupokea huduma hiyo”,ameongeza Dkt. Charido.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dkt. Amos Scott amesema THPS kupitia Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua imesaidia upatikanaji wa huduma za tohara kinga ya hiari kwa wanaume (VMMC) kama moja ya afua za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga tangu Oktoba 2021.
Dkt. Scott amesema Mkoani Shinyanga, THPS inashirikiana na AFYA Plus kutekeleza huduma za tohara katika Halmashauri zote sita, lengo ni kuongeza na kuendeleza ubora na usalama wa utoaji wa huduma za tohara tiba kwa vijana na wanaume wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ili kufikia asilimia 90% ya utoaji wa huduma hizi kwa wanaume katika Halmashauri zote zinazosaidiwa ifikapo 2026.
Ameeleza kuwa, THPS ,kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI, Kifua kikuu, kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya na UVIKO-19.
Dkt. Scott amesema mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026) unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga).
Huduma hizo ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.