Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali kujadili kuhusu utabiri wa msimu wa Masika (Machi –Mei) 2024, unaotarajiwa kutolewa tarehe 22 Februari 2024. Utabiri huu ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba, Tanga, Kilimanjaro,Arusha, Manyara,Simiyu, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kaskazini mwa Kigoma. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dar es Salaam, Tarehe 21/2/2024.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi, Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, alisema “Mkutano huu ni mwendelezo wa sehemu ya ushirikishwaji wa wanahabari katika kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa”.
Aidha aliendelea kusisitiza kuwa, uzingatiaji wa taarifa za hali ya hewa, hususan tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu na mali zao na katika kuongeza tija na ufanisikatika kupanga na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika sekta za kilimo, ujenzi, Afya, Maji, Ulinzi, Usafiri (Anga, Maji na Nchi Kavu), Madini, Utalii, shughuli za Bandari nk..
Dkt. Chang’a alisema kwa kuzingatia umuhimu huo wa huduma za hali ya hewa nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi chake imeendelea na jitihada za kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini ikiwemo uwekezaji mkubwa katika miundo mbinu ya uangazi, uchakati wa data na utabiri, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 59J. Hivyo, aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo, hali inayochangia Mamlaka kuendelea kuboresha huduma zake.
Naye Mwakilishi wa washiriki kutoka gazeti la Majira, Bi. Penina Malundo, aliishukuru TMA kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa kwa waandishi wa habari katika kuhakikisha wanaandika habari za hali ya hewa kwa ufanisi na uweledi ili wananchi waweze kuelewa.
“Utoaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari umeweza kuongeza tija kwa wananchi kufuatilia taarifa hizo katika kufanya shughuli zao hususan za kijamii”. Alisema Bi. Penina.
Katika mkutano huu, wanahabari walipata fursa ya kuona utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2024 na kutoa michango yao juu ya namna sahihi ya usambazaji wa taarifa katika kipindi chote cha msimu.