Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Lazaro Londo akifurahi na wakazi wa kata ya Malolo Wilayani Kilosa mkoani hapa mara baada ya kuwakabidhi gari.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Lazaro Londo akizungumza na wakazi wa kata ya Malolo Wilayani Kilosa mkoani hapa kabla ya kuwakabidhi gari la wagonjwa litakalowasaidia kusafirishia wagonjwa wa dharula na kuwaepusha na gharama kubwa za usafiri
Na Christina Cosmas, Morogoro
MBUNGE wa Jimbo la Mikumi Wilayani Kilosa mkoani hapa Denis Lazaro Londo amewataka wakazi wa Jimbo hilo kutambua kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitapeleka mbele yao kuanzia uchaguzi wa Serikali za mitaa wagombea mahiri na wenye uwezo wa kusimamia chama na changamoto za wananchi badala ya wale wanaokaa mbali wakisubiri kwenda kuharibu uchaguzi.
Londo amesema hayo wakati akikabidhi gari la wagonjwa katika kituo cha Afya cha kata ya Malolo ambapo amesema ni jambo jema kutatua changamoto za wapiga kura badala ya kuanza kuchafuana mitandaoni bila kutambua maendeleo yaliyopo jimboni au kwenye kata husika kwa wakati maalum.
Hivyo amewaasa wanaojaribu kumchafua mitandaoni kushindwa na kulegea na kama wanaweza watumie muda wao kwa kutatua changamoto za wakazi wa Jimbo hilo badala ya kukaa vijiweni na kubeza beza ya wenzao.
Anasema akiwa Mbunge katika miaka mitatu ya mwanzo ya awamu ya kwanza kwenye Jimbo hilo tayari ameshatumia shilingi Bilioni 2.800 kwenye kata ya Malolo pekee kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo za elimu, maji, afya na miundombinu katika kata ya Malolo pekee na kubadikisha sura ya kata hiyo.
Naye Diwani wa kata ya Malolo Iddi Kihande amewasisitiza wanaojifanya kutoona anachofanya Mbunge Londo kusafisha uso na kutoka tongotongo ili waone maendeleo yaliyopo kwa sasa Malolo badala ya kubeza.