Na Mariam Kagenda _ Kagera
Viongozi wa serikali mkoani Kagera wamehimizwa kuhakikisha wanasimamia haki za watu na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaowaonea wanyonge.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi katika maadhimisho ya kilele cha miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kagera ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa na mbunge wa Jimbo la Mvumi Livingstone Lusinde ambapo amesema kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wanawaonea watu.
Lusinde amesema kuwa wanyonge bado wanaendelea kuonewa na kudhulumiwa hivyo viongozi wanatakiwa kuhakikisha wanapambana na watu wanaowadhulumu wanyonge kwani watu wana imani na Chama Cha Mapinduzi pamoja na serikali yao hivyo hawatakiwi kuruhusu vitendo vya unyanyasaji.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa amesema kuwa katika mkoa huo serikali imeleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mkoa huo umepokea kiasi cha shilingi Bilioni 505 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Ameongeza kuwa wananchi wa mkoa huo wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kuhakikisha miradi mingi na mikubwa ya maendeleo inatekelezwa na watamlipa kwa kura nyingi ifikapo 2025 katika uchaguzi mkuu.
Katika mkoa wa Kagera kilele cha maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi yamefanyika wilaya ya Muleba ambapo yalitanguliwa na sherehe zilizofanyika kuanzia ngazi za matawi ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa chama hicho.
Mgeni Rasmi Livingstone Lusinde wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kagera
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi
Social Plugin