Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Bw. Kisena Mabuba amewaagiza Maafisa Kilimo na Watendaji wa Kata kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa mazao na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya kilimo inawanufaisha wakulima na Serikali inapata ushuru.
Hayo ameyasema leo Februari 19, 2023 katika kikao baina yake na Maafisa Kilimo, Maafisa Mifugo na Watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri . Kikao kazi hicho kililenga kujadili utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya choroko na dengu.
“Kwetu sisi mfumo wa stakabadhi ghalani utatusaidia sana katika ukusanyaji wa mapato, hatutakuwa na kukimbizana na malori yanayotoroka kwa sababu wakiuza na wakinunua mazao ,hela yetu inaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya halmashauri”alisisitiza.
Katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani unaanza mara moja, Bw. Mabuba amewaagiza Mkuu wa Division ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Afisa Ushirika kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOs) na maghala yote ya kukusanyia mazao yaliyopo katika Halmashauri na kubaini changamoto zilizopo ili ziweze kutatuliwa haraka.
Matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani ni utekelezaji wa agizo la Serikali na maazimio ya wadau wa mazao ya mikunde katika mkoa wa Shinyanga waliokubaliana kwa pamoja Februari 15,2025 kuwa mazao ya choroko na dengu yauzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili kumwinua mkulima kiuchumi. Mfumo huo utawezesha wakulima wa mazao ya choroko na dengu kuwa na uhakika wa soko na kuuza mazao yao kwa bei yenye faida na kuinuka kiuchumi pamoja na kuongeza uzalizaji wa mazao kwa tija na ubora zaidi.