Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi amefariki Dunia leo Februri 29,2024 saa 11 jioni katika Hospitali Jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu kwa ya ugonjwa wa Saratani ya Mapafu.
Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili aliingia madarakani rasmi tarehe 5 Novemba 1985.
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza msiba huo leo ambapo amesema Mzee Mwinyi alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba 2023 London Uingereza na baadaye kurejea Nchini na kuendelea na matibabu Mzena Hospital.
Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia kesho kufuatia kifo hicho.
“Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo Februari 29 saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.
Mzee Ali Hassan Mwinyi, amekuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka jana huko London, Uingereza na baadaye kurejea nchini na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena,” amesema Rais Samia.
Mkuu huyo wa nchi amesema, kutokana na kifo hicho, bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku saba kuanzia kesho Ijumaa, Machi 1, 2024.
"Ndugu wananchi, kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, ambaye amefariki dunia leo Ijumaa tarehe 29 Februari mwaka 2024 saa 11:30 jioni, katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya Mapafu.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu. Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha siku saba za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia kesho Machi 1, 2024. Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 2 Machi 2024 huko Unguja, kisiwani Zanzibar.
Inna Lillahi wa inna ilayhi raaji'un". - amesema Rais Samia
Mzee Mwinyi amefariki dunia akiwa na miaka 98 na miezi tisa na siku 21. Sawa na siku 36,091.
Mei 8, 1925, ndiyo tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa. Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga, Pwani.
Mwinyi akiwa mtoto, alipelekwa Zanzibar kusoma madrasa (elimu ya dini ya Kiislam). Tangu hapo, Mwinyi alikulia na kusoma Zanzibar hadi kufikia daraja kubwa la uongozi.
Mwaka 1933, Mwinyi akiwa na umri wa miaka minane, aliandikishwa kuanza masomo, Shule ya Msingi Mangapwani, Unguja, Zanzibar. Alisoma hapo darasa la kwanza mpaka la nne, alilohitimu mwaka 1936. Alipomaliza darasa la nne, Mwinyi alijiunga na Shule ya kati (middle school), katika Shule ya Dole. Alisoma darasa la tano mpaka la nane mwaka 1942.
Mwaka 1943, Mwinyi alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar, aliposoma ngazi ya cheti. Alitunukiwa astashahada ya ualimu mwaka 1944. Mwinyi alijiendeleza zaidi kwenye fani ya ualimu kwa kusoma Astashahada Kuu ya Ualimu (General Certificate in Education ‘GCE’), kisha Stashahada ya ualimu, kupitia Chuo Kikuu cha Durban, Uingereza.