MTOTO ALIYEPOTEZWA NA MTO MHUMBU ULIOFURIKA WAKATI AKIOGELEA BADO HAJAPATIKANA


Na Moshi Ndugulile na Mapuli Misalaba

Jeshi la zimamoto na uokoaji Wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, wanaendelea na zoezi la uokoaji kumtafuta mtoto Salum Mathew aliyesombwa na mto Mhumbu wakati akiogelea.

Mkuu wa jeshi la zimamoto na Uokoaji wa Wilaya ya Shinyanga, Inspekta Stanley Luhwago anaongoza timu ya askari wa uokoaji inayojumuisha Askari wa kuogelea na kuzamia pamoja na wananchi.

Amesema zoezi la uokozi limeanza tangu jana majira ya saa moja usiku lakini lilisitishwa kutokana na mazingira ya giza na kwamba shughuli hiyo imeendelea tena leo.

Inspekta Luhwago amesema pamoja na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika lakini nguvu kubwa ya maji ni changamoto katika shughuli hiyo ya kumtafuta mtoto huyo.

“Haya maji siyo kwamba yametuama sehemu moja haya maji yanatembea na yananguvu na katika kutembea inamaana huu mto kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mto umeongezeka upana lakini kuna sehemu tunakutana na magogo yaliyosombwa na mto kuna mashimo lakini tunaendelea kupambana kwa kuzingatia usalama”.amesema Inspekta Luhwago

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa Tambukareli Bwana Japhet Kisusi ameeleza namna alivyopata taarifa na kwamba mpaka sasa shughuli ya kumtafuta mtoto kwenye mto Mhumbu inaendelea.

“Huyu kijana inasemekana maji yamemchukua tangu jana jioni saa kumi na moja wakiwa kwenye zoezi la kuvua Samaki walikuwa wengi kutoka huko Ngokolo wenzake walipojitupia nay eye akafuata mkumbo alipojitupia basi ndiyo akasombwa na maji”.ameeleza Kisusi

Mjomba wa mtoto aliyesombwa na maji ya mto Mhumbu Bwana Abdallah Sube amesema alipata taarifa hizo jana jioni akiwa kwenye shughuli zake za utafutaji ambapo ameshukuru na kupongeza juhudi za jeshi la zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na wananchi wa Ndembezi katika juhudi za kumtafuta mtoto huyo.

Watoto waliokuwa wamefuatana na Salumu Mathew wamesema baada ya kuvua Samaki walianza kuogelea na ndipo mmoja wao alibaini kuwa maji yameanza kuongezeka lakini wakati wakijaribu kujiokoa ilishindikana Salum alisombwa na maji hayo.

Salum Mathew mwenye umri wa Miaka 12 ni mkazi wa mtaa wa Mbuyuni kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga anayesoma darasa la Nne Shule ya Msingi Bugoyi B, Manispaa ya Shinyanga. Mwenyekiti wa mtaa wa Tambukareli Bwana Japhet Kisusi akiwa kwenye eneo la tukio.


Eneo la mto Mhumbu.

CHANZO - MISALABA MEDIA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post