SHIRIKA la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF)limezindua mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa ambao ni wa miaka miwili na utatekelezwa katika kata mbili ambazo ni pamoja na Pwaga na Lupeta.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji (CDF), Koshuma Mtengeti amesema lengo la mradi huo ni kupunguza kuenea kwa vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto hasa watoto wa kike kwa kuhamasisha jamii kuzuia ukatili huo.
Amesema kupitia mradi huo, CDF itafanya kazi na watoto walioko ndani ya shule, waalimu na menejimenti ya shule, viongozi wa Serikali, wamiliki wa nyumba za kupanga , wahudumu wa afya, wazazi pamoja na vikundi vya kina baba ambavyo CDF inafanya navyo kazi katika kata hizo mbili.
"Ili kufikia malengo ya Mradi huu, CDF itafanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuwajengea uwezo watoto kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi na namna ya kuzuia ukatili wa kingono, kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waweze kutoa huduma bora na rafiki za afya ya uzazi kwa vijana balehe, kuwajengea uwezo wazazi, wamiliki wa nyumba za kupanga zilizo karibu na maeneo ya shule na walimu juu ya kulinda na kuzuia ukatili wa kingono kwa watoto, kuibua changamoto mbalimbali za ukatili wa kingono kwenye jamii, na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili kwa watoto kwa kutumia midahalo, vipeperushi, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari". Amesema Mtengeti
Aidha amesema , CDF itashirikiana na watumishi mbalimbali wa Serikali katika halmashauri ya Mpwapwa waliopo katika ofisi ya Ustawi wa Jamii, idara ya Maendeleo ya Jamii, idara ya elimu, ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Dawati la polisi la jinsia na watoto, Mahakama ya Wilaya, watendaji Kata na Vijiji kutoka kata za Lupeta na Pwaga pamoja na wadau wote wa ulinzi wa mtoto waliopo katika Wilaya ya Mpwapwa.
Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ni shirika la hiari lisilo la kiserikali, lililosajiliwa mwaka 2006 chini ya sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali namba 24/2002. Makao makuu ya shirika la CDF yapo mkoani Dar es Salaam na ofisi nyingine katika Wilaya za Tarime mkoani Mara na Mpwapwa mkoani Dodoma. Lengo kuu la shirika la CDF ni kutekeleza programu na mipango mbalimbali yenye kukuza, kutetea na kuboresha haki na ustawi wa mtoto wa Kitanzania.