Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel leo Februari, 25, 2024 amewajulia hali majeruhi wa ajali iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni, Mkoani Arusha waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru.
Dkt. Mollel amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri na mmoja ndo kapewa Rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC Mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.
"Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza majeruhi wote wa ajali hii kupatiwa matibabu bila kulipa gharama zozote",
Dkt. Mollel ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu wakati wakiendelea kuwatibia majeruhi na kwa wale waliopoteza ndugu zao utaratibu wakupatiwa miili unaandaliwa na wataalamu.
Aidha Dkt. Mollel kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu amewashukuru na kuwatia moyo watumishi wa afya katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru kwa kazi nzuri waliofanya katika kuwahudumia majeruhi wa ajali hiyo
Kwa upande wake mmoja wa majeruhi Raia wa Togo, Apelo Apeto (32) ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ubora wa Huduma waliompatia na anayoendelea kupatiwa hospitalini hapo.
"Kwa ajali hii ningekuwa nchini kwetu tayari ningekuwa nimepoteza maisha kwani kule bila kilipia huduma za matibabu hupatiwi huduma, lakini kwa Tanzania walivyowakarimu na weledi wameweza kuokoa maisha yangu mpka sasa naendelea vizuri na naweza kuongea ", ameeleza Raia wa Togo
Raia huyo amesema alikuja nchini Tanzania kwa semina ya mafunzo ya uongozi iliyokuwa ikifanyika mkoani hapo na baadaye wakaenda kufanya utalii wa kuangalia kabila la wamasai wakati wanarudi ndo wakapata ajali hiyo.
Awali akizungumza na vyombo vya Habari Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji amesema Watu 25 wamefariki dunia huku wengine 21 wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni kibaoni ikihusisha Lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.
Social Plugin