Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JICA KUISAIDIA TANZANIA KUKUZA MAWAZO BUNIFU




Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi akizungumza wakati wa hafla hiyo jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa akizungumza wakati hafla uwasilishaji wa mawazo bunifu kwa wanafunzi wa UDSM kupitia programu ya JICA Chair 2023 na programu ya Ninja Mwanamke mahususi kwa wanawake.
Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,) anayeshughulikia Taaluma Prof. Nelson Boniphace akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa licha ya kutoa shahada mbalimbali chuo hicho kinalea wanafunzi kibiashara. Leo jijini Dar es Salaam.

*************
Na Mwandishi wetu


Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) imesema itaendelea kushirikiana na Tanzania na taasisi za Elimu katika kusaidia vijana wenye mawazo bunifu ya kibiashara ili kunufaisha Taifa katika uchumi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kutafuta wazo bora la ubunifu na biashara (JICA Chair 2023,) kwa wanafunzi wa UDSM iliyofanyika chuoni hapo Balozi wa Japan nchini Tanzania Yasushi Misawa, amesema kuwa uhusiano imara wa mataifa hayo mawili utaendelea kudumishwa na kuzidi kuzalisha bunifu nyingi na za kipekee.


Aidha amesema, uwepo wa makabila takribani 130 nchini ni fursa kwa vijana kutumia TEHAMA katika kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuzingatia mila na tamaduni.


"Japan tumekuwa tukitumia mitindo ya kale na sasa katika kuboresha sekta za maendeleo, ni fursa kwa vijana na Tanzania kuendeleza biashara kwa mtindo wa Tanzania na kutanuka katika nchi nyingine." Amesema.


Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi, amesema wamekuwa wakishirikiana na UDSM katika kukuza biashara na ubunifu kwa kuwalenga vijana na wanawake kupitia programu za JICA Chair kwa wanafunzi wa UDSM na Ninja Mwanamke mahususi kwa wanawake na wanaamini hiyo ni hatua kubwa ya kuwezesha vijana kupitia mawazo yao bunifu.


Naye Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma Prof. Nelson Boniphace amesema, chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,) kinalea wanafunzi kibiashara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan, JICA pamoja na Deloitte.


"Leo tumekuwa na uwasilishaji wabunifu makundi mbalimbali wakiwemo akina Mama kupitia programu ya Mwanamke Ninja ambao kupitia mawazo yao ya ubunifu tayari wameanza kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo ni bidhaa asilia za nywele ambazo mbunifu wa bidhaa hizo aliwahi kupata athari za kiafya kutokana na kutumia kemikali katika nywele pamoja na mbunifu wa programu ya Mipango App mahususi kwa vijana na wanawake katika kusimamia mapato, matumizi na kuweka akiba." Amesema.


Kuhusiana na wanafunzi waliopo chuoni hapo amesema kuwa; UDSM imekuwa ikiendeleza mawazo ya wanafunzi kibiashara kwa kutumia changamoto kama fursa zitakazoleta matokeo chanya kwa jamii ikiwemo katika sekta za afya na mazingira.


"Licha ya kutoa degree mbalimbali Chuo kikuu cha Dar es Salaam kinafanya kazi tatu ikiwemo kufanya tafiti, kutoa huduma kwa jamii pamoja na kufanya na kuendeleza bunifu kwa kuwasikiliza na kuwapa miongozo wanafunzi wenye mawazo bunifu ya kibiashara pamoja na kuwakutanisha na watu mbalimbali wanaoweza kushiriki katika kufanikisha mawazo yao na hiyo ni kupitia Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam." Amesema.


Aidha ameishukuru Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA,) na Deloitte kwa kuendelea kukuza mawazo ya vijana kibiashara jambo litakalopunguza changamoto ya ajira pamoja bunifu hizo kuingia katika soko la Kimataifa.


Katika hatua nyingine Lilian Makoi ambaye ni mwanzilishi mweza wa Mipango App na mshindi wa Program ya Ninja Mwanamke amesema programu hiyo imewasaidia katika kuwajengea uwezo pamoja na kuboresha bidhaa ikiwemo katika kuingia ubia na kampuni nyingine na kutafuta wateja wapya.


Katika uwasilishaji wa mawazo bunifu kwa wanafunzi ( JICA Chair 2023,) Hyalosustainer. co. Ltd wameibuka kinara kupitia wazo la utengenezaji wa kemikali ya Hyaluronic Acid ambayo watumiaji huagiza nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya viwanda ikiwemo vya dawa, vipodozi na vifaa vya hospitali, huku nafasi za pili na tatu zikishikwa na mawazo bunifu ya utunzaji wa mazingira na Elimu ya afya ya uzazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com