Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Bw. Kisena Mabuba amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Kilimo kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa fedha katika maeneo yao ya kazi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato.
Agizo hilo limetolewa Februari 19, 2024 wakati wa kikao
kazi kilichofanyika katika ukumbi wa
halmashauri.
“Kwenye
suala la mapato, hatuna aibu, hali ya
mapato katika halmashauri yetu ndugu
zangu ni mbaya, mtu yeyote anayekiuka utaratibu wa ukusanyaji wa mapato ya
Serikali mkamateni na waelimisheni wananchi wajibu wajibu wao wa kutoa ushuru.....haiwezekana
halmashauri yetu kutofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.” Alisisitiza
Mabuba
amesema haridhishwi na hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo na anachukizwa
na kitendo cha mashine za kukusanya mapato kutofanya kazi vizuri. Hivyo, ameelekeza ukaguzi
wa mashine hizo ili kubaini ambazo hazifanyi kazi vizuri katika
ukusanyaji wa mapato na kuchukua hatua stahiki. Vile vile, ameelekeza ununuzi wa mashine mpya za
kukusanya mapato ufanyike ili kuendana na mahitaji halisi.
Akiainisha
vyanzo vya mapato katika halmshauri hiyo, Bw. Mabuba amesema kuwa halmashauri
hiyo pamoja na vyanzo vingine inategemea mapato ya mazao na mifugo. Kila Afisa
Kilimo, Afisa Mifugo na Mtendaji Kata asimame kwa nafasi yake na kuhakikisha
kuwa mapato ya Serikali hayapotei na kusisitiza kuwa makusanyo yote yawekwe benki
kwa wakati bila kucheleweshwa.
Aidha,
Mabuba amemwelekeza Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Edward Maduhu kuhakikisha halmashauri
inapata taarifa ya mavuno yanayoanza kuvunwa ili kuweka msisitizo wa ukusanyaji
mapato katika maeneo hayo.
Awali akielezea vipaumbele vya halmashauri wakati wa
uwasilishaji wa rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga kwa mwaka 2024/2025, Bw. Mabuba alimweleza Mkuu wa Mkoa Shinyanga kuwa halmashauri hiyo imejipanga kwa kuweka mikakati madhubuti
ambayo itasaidia kuongeza ukusanyaji wa
mapato ya Serikali. Baadhi ya mikakati aliyoiainisha ni pamoja na kufuatilia na
kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza ili kuziba mianya ya
wizi, kutoa elimu kwa wafanyabiashara,
kuandaa kanzi data ya wafanyabiashara wote, kuwezesha wakusanya mapato kwa
kuwapatia vitendea kazi muhimu na kuongeza mashine za kukusanya mapato ( POS) .