Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRAJIS AWATAKA WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI TCDC  KUJADILI HOJA KWA UWAZI

 

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume, Jijini Dodoma, (kushoto) Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Kilimo Bi. Hilda Kinanga, (kulia) Katibu wa Baraza Bi. Selestina Kinoge.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) wakifuatilia majadiliano mbalimbali ya Baraza

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ambaye pia ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amewataka wajumbe wa baraza hilo kutumia fursa hiyo kuwa wawazi, kuongea na kujadili maswala mbalimbali yatakayowasilishwa katika kikao hicho kwa maslahi ya Taasisi.

Dkt.Ndiege ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).


"Nichukue nafasi hii kuwajulisha kuwa katika kikao hiki tuko kwaajili ya maslahi ya Watumishi na kwasababu hiyo tunahitajika kuwa wawazi,kuongea na kujadili na sio kupitisha tu na kupata muafaka, kwasababu tunayokwendwa kuongea tunawawakilisha watumishi wengine wote ambao wamebaki kuendelea na majukumu mengine ya kikazi," amesema Mwenyekiti.


Aidha, aliongeza kuwa, "nichukue fursa hii kuwahimiza kwamba tumieni vizuri fursa hii, menejimenti ipo hapa kazi yao ni kusikiliza lakini pia ni kupokea, kutoa ufafanuzi kwa yale yatakayokuwa yamejadiliwa kwenye Baraza na kutekeleza ushauri utakaotolewa."


Awali Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Hilda Kinanga, aliwataka wajumbe wa kikao kutumia fursa hiyo kuimarisha mawasiliano na mahusiano mahali pa kazi, katika Taasisi na Sekta mbalimbali.

"Baraza la Wafanyakazi ni sehemu muhimu ambayo sisi watumishi tunakutana tukiwa na hadhi sawa, kwahiyo hiki ni chombo muhimu kinatakiwa kuchukuliwa kwa umuhimu wake, hivyo niwaombe wajumbe kutumia fursa hii kuendelea kuongeza mawasiliano na mahusiano katika Taasisi na kutekeleza majukumu yetu kikamilifu kwaajili ya maendeleo ya Taasisi yetu," amesema Hilda.


Mada zilizowasilishwa katika kikao hicho ni pamoja; Taarifa ya Utekelezaji ya nusu mwaka 2023/2024 pamoja na Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Taarifa ya Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Mada zingine zilizowasilishwa ni pamoja na Hoja za wafanyakazi wa TCDC kupitia TUGHE na TALGWU, Majukumu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSF), na Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Mahala pa kazi.

Katika kikao hicho wajumbe walichangia na kutoa maoni na mapendekezo katika mada mbalimbali zilizowasilishwa ambapo wameipongeza Menejimenti ya TCDC kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuwapatia vitendea kazi pamoja na kuanza kuboresha maslahi ya watumishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com