Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai |
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai amewashauri Wananchi kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira kama jitihada za kupambana na Umaskini.
Amesema hali ya umaskini imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira kupitia shughuli za kibinadamu, jambo linalopelekea athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
Ndugai ameeleza hayo Februari, 09, 2024 kwenye hafla ya kumpa mkono wa kwaheri aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remidius Mwema ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Manyara.
Amesema,tabia ya umaskini inatokana na kuharibu mazingira na kueleza kuwa watu matajiri huwa hawana tabia ya uharibifu wa mazingira .
Ndugai pia ametumia nafasi hiyo kumuomba Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon Mayeka kuwasaidia wananchi, kupiga vita umaskini na uharibifu wa mazingira kama kipaumbele kikuu cha kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kongwa.
"Mimi kama mwakilishi wa wananchi nakuomba eneo moja tu la kufanyia kazi; nalo ni maendeleo ya uchumi wa watu wa Kongwa"amesema
Akizungumza katika sherehe hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Remidius Mwema Emmanuel amesema, ataendelea kuikumbuka Wilaya ya Kongwa kwa mambo mengi ikiwemo ushirikiano wa viongozi uliopelekea ukamilishaji wa miradi ya maendeleo kwa Wakati na kuibuka kuwa kinara ngazi ya Taifa.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon Mayeka amewataka Wananchi wilayani Kongwa kudumisha umoja katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ili kuendeleza kasi ya uwajibikaji katika taasisi mbalimbali.
Sambamba na hilo amewataka wananchi kuunga mkono Jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya hifadhi za barabara zinazopita katika makazi yao badala ya kuzitegemea taasisi sinazohusika na ujenzi wa barabara.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa White Zuberi amesema mchango wa Mwema kuhusu kutangaza historia ya harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika umeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya viashiria vimeanza kuonekana.
Viashiria hivyo ni pamoja na kufanyika kwa Ukarabati wa handaki lililotumiwa na wapigania uhuru sanjali na mpango wakufanyika kwa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mwaka 2024, kufanyika Wilayani Kongwa.
Aidha hafla hiyo iliandaliwa na kamati maalumu kwa usimamizi wa Katibu tawala Wilaya Bi. Sozi Ngate ambapo wakuu wote wa wilaya walipewa zawadi mbalimbali kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii ukiwemo uongozi wa Chama Cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kongwa, Wafugaji, Wakulima na watumishi.
Social Plugin