NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amefanya ziara ya kutembelea mradi wenye thamani ya Shilingi 422 milioni wa ujenzi madarasa Saba na matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari ya Mazoezi Chang'ombe iliyopo ndani ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam(DUCE). ambapo ameupongeza uongozi wa Chuo kuhakikisha ujenzi unakwenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Februari 20, 2024 RC Chalamila amesema uongozi wa shule umejitahidi kusimamia ujenzi wa mradi huo na kuhakikisha fedha ambazo zimetolewa na serikali zinalenga katika ameneo yaliyokusudiwa.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyobora ndo maana wamekuwa wakijitahidi kuboresha madarasa na vyoo katika shule mbalimbali nchini ili kumuondolea changamoto mwanafunzi.
"Wengine wanaishi mbali na shule wanazoenda kusoma, tumekuja na mpango wa kujenga hosteli kila shule, kwanza kujenga nidhamu ya taaluma kwa wanafunzi". Amesema
Aidha amesema wameanzisha mpango wa kujenga hosteli za wanafunzi kwa shule zote ili kujenga nidhamu ya taaluma na kutengeneza mazingira mazuri ya kujadili kuhusu kesho yao.
Ambapo amesema mpango huo utaenda sambamba na kujenga shule maalum kwa ajili ya Wanafunzi wanaopata sifuri kwenye mitihani yao ya mwisho itakayosajiliwa kwa mfumo wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Awali, akisoma taarifa za shule hiyo Rasi wa Chuo cha DUCE, Profesa Stephen Maluka amesema madarasa hayo saba yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa.
"Tuna wanafunzi wengi zaidi ya 1000 na idadi imekuwa ikiongezeka kutokana na uhitaji na haya madarasa Saba yataweza kuchukua wanafunzi 180 na ujenzi wake ulianza mwaka 2019 umekuwa ukienda taratibu kwakuwa tunategemea fedha kutoka mapato ya ndani na Serikali," amesema