SERIKALI MAPINDUZI ZANZIBAR WAISHUKURU PUKA KUKARABATI MAJENGO, UJENZI MATUNDU YA VYOO SHULE YA KISIWANDUI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo yaliyofanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na ujenzi wa matundu ya choo katika  Shule ya Msingi Kisiwandui Zanzibar.

*****************

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeishukuru Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania kwa kuamua kufanya ukarabati mkubwa wa majengo ya madarasa na ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Kisiwandui ambapo kampuni hiyo imetumia Sh.milioni 130 kufanya ukarabati huo.

Akizungumza leo Februari 20,2024 wakati wa uzinduzi wa majengo hayo yaliyokarabatiwa katika shule hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa amesema wnathamini na kutambua mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo katika kustawisha sekta ya elimu Zanzibar.

Amesema pamoja na Serikali kuendelea kujenga miundombinu ya elimu ili kuleta maendeleo endelevu ya jamii, michango ya wadau wa elimu kutoka sekta binafsi na umma ni muhimu kwa kuwa inasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi.

“Naipongeza Kampuni ya mafuta ya Puma kwa kufanikisha ukarabati wa majengo ya madarasa na kujenga vyoo vya shule hii kwani inakwenda kuongeza haiba ya shule na kuondoa changamoto ya wanafunzi kujifunza katika mazingira duni.

“Natambua mwaka jana mlitusaidia kwenye programu ya kukuza ujuzi na ajira kwa wanafunzi wa Chuo cha Karume na mwaka huu mmekuja na maajabu haya, huu ni mfano wa kuigwa na kila mpenda maendeleo ya elimu”, amesema.

Ameongeza kuimarishwa kwa miundombinu ya shule hiyo yenye wanafunzi wenye mahitaji maalum kutaongeza ari ya wanafunzi kujifunza na wazazi kuwatoa watoto wao majumbani ili waweze kupata haki ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.

Amesema kuwa Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye uhitaji maalumu na kujitahidi kuziondoa na kwa kutambua hilo, Serikali ya awamu ya nane imeanzisha vituo maalum vinavyotoa elimu mjumuisho viliopo Jendele kwa Unguja na Pujini kwa Pemba.

Aidha ameiomba Puma Energy na wadau wengine kuona namna wanavyoweza kuvisaidia vituo vinavyohudumia watoto wenye mahitaji maalumu kwani bado vina mahitaji makubwa.

Awali akitoa salamu za kampuni ya Puma Energy, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Fatma Abdallah amesema kiasi cha Sh.milioni 130 kimetumika katika kukarabati majengo ya madarasa na ujenzi wa matundu ya vyoo vya shue hiyo.

Amesema kuwa ufadhili wa ukarabati huo ni sehemu ya mipango ya kampuni hiyo kurejesha kwa jamii faida wanayoipata na kwa mwaka huu wameona ni muhimu kutumia fedha hizo kwa shule hiyo kutokana na upekee uliopo.

“Puma Energy imeanzisha mradi wa ‘energizing school communities’ ili kuunga mkono maendeleo ya sekta ya elimu na kuhamasisha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi ili kuimarisha matokeo ya wanafunzi.”

Aidha ameeleza azma yao ya kuendelea kuwekeza Zanzibar kwa kujenga vituo zaidi vya mafuta katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ili kutanua wigo wa biashara na huduma kwa wananchi.

Pia amewapongeza walimu na kamati ya maendeleo ya shule hiyo kwa kumpa ushirikiano mkandarasi aliyetekeleza mradi huo na kuukamilisha jkwa wakati.

Wakati huo huo akitoa taarifa ya shule hiyo Mwalimu Maryam Ameir amesema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1955 kwa sasa ina wanafunzi 2024 wakiwemo 70 wenye ulemavu mbali mbali.

Amesema ukarabati huo uliohusisha uwekaji wa dari, sakafu, rangi, uimarishaji wa kuta, ujenzi wa kibanda cha walinzi na vyoo vikiwemo vya wenye ulemavu, umeondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili awali ikiwemo ya vumbi.

Amesisitiza hatua hiyo itaimarisha ari ya kujifunza kwa wanafunzi na kufundisha kwa walimu hivyo kuimarisha ufaulu katika mwaka huu kwa kuondoa ufaulu wa alama D baada ya kufanikiwa kuondoa ufaulu wa alama F katika mitihani iliyopita.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisiwandui Ally Mahmoud amesema msaada huo uliotolewa na kampuni hiyo imeifanya shule yao kuwa na matundu ya vyoo 20, hivyo kuweka uwiano baina ya idadi ya wanafunzi na idadi ya vyoo kama ilivyo kwenye muongozo wa wizara ya elimu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa( kulia) akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa majengo ya Shule ya Misingi Kisiwandui Zanzibar baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa sambamba na ujenzi wa matundu ya choo uliofanywa na Kampuni ya Mafuta ya Puma katika shule hiyo ambapo Sh.milioni 130 zimetumika.Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Fatma Mohamed Abdallah( wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu , Maandalizi na Msingi Zanzibar Fatuma Mode  ( wa kwanza kushoto).
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa( kulia) akivuta kitambaa baada ya  kuzinduliwa kwa majengo ya Shule ya Misingi Kisiwandui Zanzibar baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa sambamba na ujenzi wa matundu ya choo uliofanywa na Kampuni ya Mafuta ya Puma katika shule hiyo ambapo Sh.milioni 130 zimetumika.Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Fatma Mohamed Abdallah( wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu , Maandalizi na Msingi Zanzibar Fatuma Mode  ( wa kwanza kushoto).
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa( kulia) akisapeana mkono na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania wakati wa uzinduzi wa majengo yaliyofanyiwa ukarabati pamoja na ujenzi wa matundu ya choo katika  Shule ya Misingi Kisiwandui Zanzibar.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Fatuma Abdallah akizungumza wakati wa uzinduzi wa majengo yaliyofanyiwa ukarabati pamoja na ujenzi wa matundu ya choo uliofanywa katika Shule ya Msingi Kisiwandui Zanzibar ambapo kampuni hiyo imetumia Sh.milioni 130 katika kufanya ukarabati huo
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhamed Mussa( kulia) akivuta kitambaa baada ya  kuzinduliwa kwa majengo ya Shule ya Msingi Kisiwandui Zanzibar baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa sambamba na ujenzi wa matundu ya choo uliofanywa na Kampuni ya Mafuta ya Puma katika shule hiyo ambapo Sh.milioni 130 zimetumika.Kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Fatma Mohamed Abdallah( wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu , Maandalizi na Msingi Zanzibar Fatuma Mode  ( wa kwanza kushoto).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post