SHULE YA EL-SHADDAI YAWASHIKA MKONO WATHIRIKA WA MAAFA HANANG



NA. MWANDISHI WETU

Uongozi wa shule ya Msingi  El shaddai  iliyopo Dodoma umekabidhi misaada ya kibinadamu ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti kutoka mlima Hanang’ yaliyotokea tarehe 3 Disemba 2024 mkoani Manyara.
Akipokea msaada huo  23 Februari, 2024 kwaniaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi,  Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jane Kikunya amesema Ofisi inatambua mchango mkubwa wa Taasisi zinazoendelea kushiriki katika kurejesha hali kwa waathirika wa maafa hayo kwa namna wanavyoendelea kutoa misaada mbalimbali ili kusaidia hatua ya urejeshaji hali inayoendelea.

"kipekee kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu naomba kuwashukuru kwa moyo mliouonesha na nia katika kuchangia na kutoa msaada kwaajili ya waathirika wa maafa, tunashukuru kwa Shule yenu kwa kujitokeza na kuchangia misaada muhimu kwaajili ya waathirika wa Hanang, misaada iliyotolewa itawafikia waathirika wote kwa utaratibu uliowekwa na Ofisi."amesema  Jane Kikunya.

Ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kurejesha hali za waathirika wa maafa hayo yaliyosababisha vifo, uharibifu wa makazi, miundombinu ya barabara, umeme na mashamba, huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha hatua zilizopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule hiyo   Juliana Kallinga amesema uongozi wa shule na wafanyakazi wa shule hiyo wameandaa baadhi ya vitu ambavyo ni ishara ya kuwafariji waathirika hao.

"Kama familia ya El-Shaddai tunapenda kuwafariji Watanzanaia wenzetu walioathirika kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo mbalimbali kwa wakubwa na wadogo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia,lakini pia tunamuomba Mungu aendelee kuwapa mfaraja na nguvu kila aliyepotelewa na ndugu jamaa na marafiki, hakika shule yetu iliguswa na changamoto hii."amesema Juliana.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post