Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Godfrey Malekano wakionyesha hati za ushirikiano wa kuwainua wakulima na wajasiriamali wadogo wa sekta ya kilimo katika hafla iliyofanyika mwisho mwa wiki iliyopita makao makuu ya Benki ya CRDB
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Godfrey Malekano wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kuwainua wakulima na wajasiriamali wadogo wa sekta ya kilimo katika hafla iliyofanyika mwisho mwa wiki iliyopita makao makuu ya Benki ya CRDB.
---
Dar es Salaam. Tarehe 18 Februari 2024: Katika kuendeleza jitihada za kuwainua wakulima na wajasiriamali wa biashara ya mazao ya kilimo nchini, taasisi ya CRDB Bank Toundation imesaini Mkataba wa ushirikiano na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Tume ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema mchango wa kilimo nchini ni mkubwa kuanzia kwenye uzalishaji wa chakula mpaka utoaji wa ajira hasa kwa wanawake na vijana, makundi yanayopewa kipaumbele na taasisi anayoiongoza.
“Azma ya taasisi yetu ya CRDB BaNK Foundation ni kusaidia kuongeza ujumuishi wa kiuchumi, kuboresha maisha, na kukuza ustawi wa jamii yetu. Ili kufikia malengo haya CRDB Bank Foundation imekuwa ikibuni na kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji kama vile program ya IMBEJU ambayo hadi sasa imeweza kuwafikia wanawake zaidi ya 125,000 na kutoa mitaji wezeshi zaidi ya Shilingi Bilioni 5,” amesema Tully Esther.
Mkurugenzi huyo pia ameongeza kuwa CRDB Bank Foundation itashirikiana na mdau yeyote anayelenga kuwakomboa kiuchumi vijana na wanawake ilikuwapa nafasi ya kuujenga uchumi wa taifa.
“Ushirikiano huu unajielekeza zaidi kwenye sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa zaidi ya asilimia 75 kwa Watanzania na kuchangia asilimia 26 kwenye pato la taifa huku kikituhakikishia chakula kwa asilimia 95. Katika wilaya, tunatarajia kuzifikia walau Amcos (vyama vya ushirika) 10 ambavyo tutaviwezesha kwa kati ya Shilingi milioni moja mpaka shilingi milioni 30 au zaidi ya hapo kulingana na mahitaji yatakayokuwepo. Mkakati huu tunaamini utasaidia kukuza biashara ya wakulima na wajasiriamali wa kilimo,” amesema Tully Easther.
Wakati CRDB Bank Foundation ikitarajiwa kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali pamoja na mtaji wezeshi, TCDC itaratibu upatikanaji wa vyama hai vya ushirika huku WRRB ikihakikisha uhifadhi makini wa mazao ya kilimo na TMX likiwakutanisha wakulima na wanunuzi wa mazao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX, Godfrey Malekano amesema jukumu lao hasa ni kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri ya mavuno yake. Tangu mwaka 2018 soko hilo lililpoanzishwa, amesema wameshayasajili mazao kadhaa ukiwamo ufuta, dengu, korosho, mbaazi na mazao ya mifugo na sasa hivi wanakamilisha utaratibu wa kuingiza madini.
“Soko linaendesha shughuli zake kwa kutumia teknolojia. Sio lazima muuzaji na mnunuzi waonane. Kwa mkulima aliye mahali popote nchini, anaweza kuyaunza sokoni kwetu iwapo ameyapeleka kwenye ghala linalotambulika. Sio lazima mnunuzi na muuzaji waonane, teknolojia inawaunganisha watu hawa. Ushindani unafanyika kwa uwazi wa hali ya juu na mkulima anapata bei nzuri zaidi sokoni,” amesema Malekano.
Soko hilo pia, Malekano amesema linampunguzia mkulima gharama kwani anachotakiwa ni kuyapeleka mazao yake ghalani badala ya sokoni ambako si lazima amkute mnunuzi kwa wakati huo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya Benki ya CRDB, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege amesema kuna zaidi ya vyama 7,000 vya ushirika nchini ambavyo sasa vitaanza kunufaika na mkakati uliowekwa na wadau wanaoenda kuutekeleza.
Mtendaji Mkuu wa WRRB, Asangye Bangu amesema huu ni mwendelezo wa kuwainua wakulima nchini. “Nguvu za kila mmoja wetu kwenye ushirikiano huu ni kubwa. Tunaenda kuyatekeleza yote tuliyokubaliana hapa kumnufaisha mkulima wa Tanzania,” amesema Bangu.
Social Plugin