Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YAWATAKA WAFANYABIASHARA NA WAZALISHAJI WA VYAKULA NCHINI KUZINGATIA USALAMA WA CHAKULA



Kaimu Meneja wa Kitengo cha kufanya Tathimini ya vihatarishi vya chakula (TBS) Dkt.Ashura Katunzi akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13, 2024 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam

************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Vyakula nchini kuzingatia usalama wa bidhaa hizo kabla ya kumfikia mlaji kwa lengo la kulinda afya kwa mlaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13,2024 Kaimu Meneja wa Kitengo cha kufanya Tathimini ya vihatarishi vya chakula (TBS) Dkt.Ashura Katunzi amesema usalama wa chakula ni wajibu wa kila mtu katika mnyororo wa thamani,kuanzia kwa mzalishaji hadi kinapomfikia mlaji.

Amesema kuwa chakula kisipokua katika hali ya salama kinaweza kusababisha madhara ya kiafya na hata  kusababisha vifo na kuzorotesha uchumi pamoja na maendeleo ya watu.

Dkt. Katunzi amebainisha mbinu zitakazosaidia kuwa na chakula salama ambapo amesema katika maandalizi ya chakula migahawani na Viwandani waandaji wanapaswa kuweka mazingira safi na kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya maandalizi hayo.

Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutenganisha chakula kibichi na kilicho tayari kuliwa, kwa sababu kile kilichopikwa kitakuwa kimezingatia kanuni za usafi "huwezi kuchanganya nyama iliyopikwa na nyama mbichi katika friji. Dkt. Katunzi ameeleza

Pamoja na hayo ameeleza kuwa chakula kinatakiwa kuhifadhiwa katika joto salama ili kuhakikisha hakizalishi vimelea vya wadudu na kutumia malighafi ambazo ni bora kwa lengo la kulinda afya ya mlaji.

"Wenzetu wale wanaofuga wanyama wasiende kuuza wanyama wakiwa na siku chache wametumia madawa, wataalamu wanaeleza mnyama aliepewa dawa akae muda gani nyama yake iweze kuliwa. Na wale wanaolima matunda na mboga yakipelekwa sokoni, mlaji anaweza asijue mboga hii imepuliziwa dawa kwa muda gani". Amesema Dkt. Katunzi.

Kwa Upande wake Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria (TBS) Bw. Moses Mbambe amesema kuwa sheria inawataka wazalishaji wa chakula kuzingatia viwango   na waagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi kusajili maeneo ambayo usindikaji wa bidhaa husika unafanyika ili kuhakikisha ubora na usalama.

Aidha Meneja ukaguzi huyo ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizo wanaofanya ulaghai  kwa kuuza bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umepita, kuachana na tabia hiyo kwa kuuza bidhaa ambazo hazijazingatia mahitaji ya viwango.

Kaimu Meneja wa Kitengo cha kufanya Tathimini ya vihatarishi vya chakula (TBS) Dkt.Ashura Katunzi akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13, 2024 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam
Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria (TBS) Bw. Moses Mbambe akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13, 2024 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com