Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Kikundi cha Team February cha mkoani Shinyanga kimefanya matendo ya huruma kwa kutoa msaada katika kituo cha malezi ya watoto Saint John Bingen Home of Children kilichopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Wametoa msaada huo leo Februari 29, 2024 katika kituo cha malezi ya watoto Saint John Bingen Home of Children kilichopo kata ya Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Akitoa shukrani mara baada ya kupatiwa msaada huo msimamizi wa kituo cha malezi Saint John Bingen Home of Children Esta Livision amewashukuru Team February kwa kuwakumbuka watoto wenye uhitaji katika kituo hicho.
"Kituo cha malezi ya watoto Saint John Bingen kilianzishwa mwaka 2022 kikiwa na watoto watano ambapo mpaka sasa tuna watoto 39, malengo ya kituo chetu ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu, changamoto ni nyingi kama vile mahitaji mbalimbali ikiwemo mafuta maalum ya kujipaka kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi, mashine ya kufulia nguo, mavazi, vifaa vya kujifunzia ikiwemo daftari pamoja na mahitaji mengine,"amesema Esta Livision.
"Awali tulikuwa na tv mmoja tu ambayo tulikuwa tukitumia kuangalia watu wote tunashukuru kwa hiki mlichotupatia ni moyo wa upendo mliouonesha kwa watoto hawa kupitia sadaka hii Mungu akawabariki sana, zipo sehemu nyingi zenye uhitaji lakini mmetuona sisi, tunashukuru sana", ameongeza Esta Livision.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Team February Eva Chaulema amesema moja ya jukumu la umoja wa kikundi hicho ni kusaidia, kushirikiana na kuungana na jamii kwenye mambo mbalimbali sambamba na kusherehekea mfano wa siku ya kuzaliwa kwa pamoja na wale waliozaliwa mwezi wa pili.
"Sisi kama Team February kwa umoja wetu tumefika katika kituo hiki kwa ajili ya kujumuika na kusherehekea pamoja na watoto wetu, ni moja ya jukumu letu kuungana na kuisaidia jamii lakini pia kusherehekea pamoja katika mwezi huu wa pili, tunawakabidhi Flat Screen inchi 43 pamoja na king'amuzi cha Azam Tv kwa lengo la kusherehekea pamoja", amesema Eva Chaulema.