WAKASUVI AMEFIKWA MAUTI KATIKATI YA JUKUMU ZITO: DK. NCHIMBI


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Ndugu Hassan Mohamed Wakasuvi ni pigo kubwa, si kwa mkoa huo pekee, bali Chama, Serikali na taifa zima kwa ujumla, ambapo amefikwa na mauti akiwa ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo, iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Nchimbi amesema kuwa Komredi Wakasuvi alikuwa mmoja wa viongozi shupavu wa Chama Cha Mapinduzi, kuanzia mkoani kwake, hadi ngazi ya taifa, ambapo kutokana na uwezo na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na ushirikiano tangu alipochanguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM, mwaka 2007, aliendelea kuaminiwa hadi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, nafasi aliyokuwa nayo hadi mauti yalipomfika.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi kwenye msiba wa Mzee Wakasuvi, kabla ya mazishi ya kiongozi huyo, Jumamosi Februari 24, 2024, katika Kijiji cha Mabama, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kiwango cha kuaminiwa Mzee Wakasuvi kilikuwa ni kikubwa sana. Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Mkoa na Mjumbe wa NEC ya CCM Taifa, pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Lakini pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyopewa jukumu la kuangalia namna ya kukiboresha chetu. Makamu wake alikuwa ni Mzee Wassira (Steven).

“Wanauliza watu maswali mbalimbali. Mimi ilikuwa imepangwa niwatembelee na kuonana nao Jumatatu (keshokutwa). Wakaniulize maswali waliyopanga kuniuliza nami nilikuwa nimejiandaa kwenda kujibu maswali hayo,” amesema Dk. Nchimbi na kuongeza;

“Ameanza uongozi muda mrefu sana tangu Umoja wa Vijana. Wenzake wengine wako hapa akina Mzee Lukuvi (William), Mzee Luhavi (Rajabu) na wengine. Muda wote alikuwa anahamasisha maendeleo ya nchi yetu na kuchochea uimara wa CCM. Chama kimepoteza, Serikali imepoteza na Wananchi kwa ujumla wamepoteza kiongozi mahiri na shupavu. Tuna kila sababu ya kulinda na kuenzi kazi zake, kwa kuendelea umoja, kushikamana, amani na utulivu thabiti bila kujali tofauti zetu za kisiasa, dini, kabila wala maeneo.”

Mbali ya salaam hizo, Dk. Nchimbi pia aliwasilisha salaam za Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo Katibu Mkuu wa CCM huyo amesema kuwa msiba huo umemgusa Mheshimiwa Rais moja kwa moja lakini hakuweza kuhuduria kutokana na ratiba ya majukumu mengine ya kikazi, nje ya nchi.

“Kama ambavyo imekuwa kawaida kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kila kunapojitokeza jambo kama hili, hapa pia amejitoa kwa uzito mkubwa tangu tu zilipotokea taarifa za msiba huu. Washauri wake wa siasa wote wako hapa. Pia ametutuma sisi wasaidizi wake, Mhe. Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali na mimi kwa upande wa Chama kuleta salaam zake za pole kwa wanaCCM wote na Tabora kwa ujumla wenu. Nasi pia tutafikisha salaam na shukrani zenu mlizompatia yeye kwa jinsi alivyojitoa kushiriki katika msiba huu,” amesema Dk. Nchimbi.

Mzee Hassan Mohamed Wakasuvi alifikwa na mauti siku ya Alhamis, Februari 22, 2024, baada ya kuugua kwa muda mfupi, ambapo pia alikuwa katika maandalizi ya kusafiri kikazi kwenda mkoani Pwani, Jumapili, Februari 25, 2024 kwa ratiba ya majukumu mengine ya kazi za Chama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post