NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WANANCHI wamelalamikia mfumo wa kutoa maoni kwenye Dira ya Taifa ya 2050 kuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambapo wamependekeza kuundwa kwa mfumo mbadala wenye uwazi ambao utasaidia watu kutoa maoni yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 28,2024 wakati wa Semina za Jinsia na maendeleo ambazo hufanyika kila Jumatano katika Ofisi za TGNP- Mtandao Jijini Dar es Salaam, Mwezeshaji Bw. Ocheck Msuva amesema wananchi wameonesha shauku ya kutambua Dira iliyopita ya 2025 na wametamani kuona mambo mapya katika Dira ya 2050.
Ameeleza kuwa wananchi wameona ni muhimu sauti za pamoja zikiandaliwa ili kuwakilishwa kama sauti mbadala ambapo itasaidia kuzipa nafasi kwa jamii ambayo haijafikiwa na kutokuwa na ufahamu kuhusiana na suala la dira.
Amesema kuwa wananchi waliohudhuria warsha hiyo wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kwa jamii inayowazunguka hasa katika kuwafahamisha kuhusiana na suala zima la dira ya Taifa ili jamii itoke usingizini.
"Dira ya Taifa 2025 imewapa muamko mkubwa sana kumbe baadhi ya mambo wanayoyaona wanaweza kuhoji kwa kuangazia nini kilisemwa kupitia dira". Amesema Bw. Msuva.
Kwa Upande wake Mwanaharakati wa Jinsia kutoka kata ya Majohe Bi.Winfrida Gerald amesema kuwa anakwenda kuwafahamisha wananchi wa mazingira yake anayoishi kwa lengo la kuhakikisha mawazo yao yanafika katika Dira ya 2050.
Nae ,Mdau wa semina za Jinsia na maendeleo Bw. Kennedy Anjelita amesema katika Dira ya Taifa ya ya 2050 ni vema wakisikiliza maoni ya wananchi ambapo itakuwa ni kilimo cha uwajibikaji kuwapima viongozi kulingana na Dira.