NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa semina za jinsia na maendeleo wamepewa semina yenye lengo la kuchochea msukumo kwa watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi na kuondokana na dhana potofu kwa kuachia masomo hayo jinsi moja pekee.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 14,2024 katika semina hiyo iliyofanyika makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mabibo-Dar es Salaam, Mhadhiri wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) Dkt. Promota Haule amesema mchango wa wanawake wanasayansi unatambuliwa na wanapewa kipaumbele.
Aidha Dkt. Haule amesema kuwa anatarajia muamko mkubwa kwa wajumbe waliohudhuria semina hiyo kuwa mabalozi kwa kutoa hamasa majumbani kwao na maeneo mbalimbali kwa watoto kupenda masomo ya sayansi.
"Wajumbe wengi watakuwa wadau wakienda kuhamasisha mabinti majumbani kwao kupenda masomo ya sayansi na baadae waje wafanye kazi za kitaalamu katika tasnia hii ya Sayansi". Amesema
Pamoja na hayo ameeleza kuwa mabinti,walezi na jamii kwa ujumla wamekuwa na dhana ya kuwa masomo ya sayansi ni magumu na kutoyapa kipaumbele.
"Ukisoma masomo ya sayansi ni magumu,ni ya wanaume, pengine ukisoma masomo hayo ajira hata hamna kwahiyo wanakuwa na fikra hizo". Dkt. Haule ameeleza.
Vilevile ametoa wito kwa jamii kutoa hamasa kwa mabinti kuyapenda masomo sayansi ambapo wakifanikiwa watakuwa bora kiuchumi na kusaidia Taifa katika maendeleo.
"Wanaweza kuwa wauguzi,mabwana shamba,Sayansi ni Pana watakapo kuwa katika kazi hizo watapata kipato lakini Taifa litapata maendeleo,Taifa bila maendeleo haiwezi kupiga hatua kwahiyo ni muhimu tuhakikishe kwamba tunapata wanawake ambao watakujakutia chachu katika maendeleo ya nchi yetu". Amesema
Kwa upande wake,Mdau wa semina za Jinsia na Maendeleo kutoka Kata ya Mburahati Bw.Alan Christopher amesema mfumo dume umechangia kwa asilimia kubwa kwa wanawake kutojihusisha na masomo ya sayansi kutokana na nadharia yakuwa ni kazi ngumu zinazomfaa mwanaume.
Aidha amesema kuwa lishe duni imekuwa ni sababu mojawapo inayopelekea mabinti kufanya vibaya katika masomo ambapo ameeleza kwamba yeye atakua kielelezo kwa familia yake kuhakikisha mabinti wanafanya vizuri na kufanikiwa katika masomo ya sayansi.
Nae, Mwanaharakati wa masuala ya jinsia Bw.Joshua Deus ameeleza kuwa sababu inayopelekea mabinti wengi kutojihusisha na masomo ya sayansi ni kupewa kazi nyingi za nyumbani tofauti na watoto wa kiume ambapo hupelekea mtoto wakike kukosa nafasi ya kujisomea anapokuwa nyumbani.
Semina hiyo imebeba dhima isemayo"NI KWA NAMNA GANI MCHANGO WA MWANAMKE MWANASAYANSI UMETAMBULIKA NA KUPEWA KIPAUMBELE "imekusudia kuinua watoto wakike kupendelea masomo ya sayansi.
Social Plugin