Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Dkt Yahaya Nawanda wakati wa Uzinduzi rasmi wa mradi wa Afya Thabiti Mkoani Simiyu na Mara uliofanyika Simiyu.
**
Simiyu Machi 7, 2024 – Shirika la Amref Health Africa Tanzania (Amref) limezindua mradi wa “Afya Thabiti” unaolenga kuendeleza huduma za VVU/UKIMWI. Dhumuni la Mradi ni kuwekeza katika mifano dhabiti ya kimafanikio, ushirikishwaji wa jamii husika katika kujikinga na maambukizi ya VVU na matibabu katika vituo vya afya na jamii za Mara, Simiyu na Zanzibar wakati huo huo kudhibiti mifumo ya kuimarisha mifumo ya afya katika kudhibiti maambukizi.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kupambana na janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030 na unafadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) nchini Tanzania. Mradi pia utafuatilia na kutathmini na kufuatilia usimamizi, ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za VVU.
Mradi huo wa miaka mitano wa “Afya Thabiti” unatekelezwa na Amref Health Africa Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Afya, Elimu na Usalama wa Mazingira Tanzania (Ciheb-Tz), Kituo cha Mawasiliano na Maendeleo Tanzania (TCDC) na Afya Plus kwa miongozo ya PEPFAR na Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na VVU/UKIMWI (UNAIDS) malengo ya kasi ya 95-95-95 ifikapo mwaka 2030. Mradi huu utahakikisha kuwa asilimia 95 ya Watu Wanaoishi na VVU(WAVIU) wanajua hali zao, 95% kati yao wako kwenye matibabu ya kudumu, na 95% wamefubaza virusi vya Ukimwi mwilini.
Uzinduzi rasmi wa mradi wa Afya Thabiti ulizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Dkt Yahaya Nawanda na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, wawakilishi wa wadau wa maendeleo (PEPFAR-CDC), wafanyakazi wa Amref Health Africa, asasi za kiraia, washirika wa utekelezaji, viongozi wa kidini wa kikanda, jamii, na sekta binafsi.
Dkt. Yahaya Nawanda alisisitiza umuhimu wa mradi huo katika kuendeleza mapambano dhidi ya kupunguza maambukizi, na kudhibiti maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI katika mkoa wa Simiyu. Ameeleza kuwa kumekuwepo na kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka asilimia 3.9 katika Utafiti wa Athari za VVU Tanzania (THIS) 2016/2017 hadi 3.7% katika MWAKA 2022/2023 na kushukuru juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na VVU/UKIMWI mkoani Simiyu.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, alisisitiza haja ya kudhibiti na kupunguza maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI kwa kuzingatia malengo ya kitaifa na kimataifa ya 95-95-95. Haya yanajiri baada ya matokeo ya Utafiti wa Athari za VVU Tanzania (THIS) mwaka 2022/2023 kubainisha kuwa kiwango cha maambukizi mkoani Mara ni 5%, juu ya kiwango cha kitaifa cha 4.4%. Mtanda alisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa ushirikiano na mashauriano ili kuboresha mipango ya utoaji wa huduma za VVU/UKIMWI katika mkoa huo.
Dkt George Mgomella, Mkurugenzi wa miradi kutoka CDC Tanzania, akimwakilisha Mkurugenzi mkazi wa kituo cha Serikali ya Marekani cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa, Dkt Mahesh Swaminathan (U.S CDC Tanzania), alipongeza hatua iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya VVU katika mikoa ya Mara, na Simiyu. CDC imeitaka mikoa hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukabiliana na ugonjwa huo. PEPFAR, kupitia CDC, inatoa kipaumbele kwa juhudi za kupanua programu za kuzuia VVU na matibabu kwa msingi wa ushahidi wa afya katika maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi nchini Tanzania. Serikali ya Marekani inatambua Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI), viongozi wa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, na mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kiraia kwa kujitolea kwao kuboresha matokeo ya afya nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Amref Health Africa nchini Tanzania Dkt. Florence Temu, mradi wa Afya Thabiti unalenga kuongeza idadi ya watu wanaoishi na VVU/UKIMWI wanaojua hali zao kupitia upimaji wa VVU na kutoa matibabu ya muda mrefu na endelevu ya dawa za kurefusha maisha. (ART) na upimaji wa virusi ili kuhakikisha wamefubaza virusi.
Mradi utatoa huduma za upimaji wa VVU, kuunganisha WAVIU wapya katika dawa huduma za ART, kutoa kinga na matibabu ya hali ya juu kwa WAVIU, kutoa huduma za hali ya juu za tohara kwa kuzuia VVU, na kuongeza afua za ubunifu na madhubuti za kuzuia na matibabu ya VVU kwa watu walio katika hatari. Zaidi ya hayo, mradi utaimarisha ripoti za ufuatiliaji na tathmini (M&E), ufuatiliaji wa kimatibabu, na matumizi ya data ili kuboresha utendaji wa programu.
Mradi wa Afya Thabiti ni mojawapo ya mipango ya afya ya Amref nchini Tanzania ili kuunga mkono juhudi za serikali na wadau wengine wa afya katika kupambana na kudhibiti maambukizi ya VVU / UKIMWI. Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya UKIMWI wa THIS wa mwaka 2022/2023, wastani wa kiwango cha maambukizi ya VVU miongoni mwa watu wenye umri kati ya miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.4 nchini, yaani katika kila watu 100, watu 4 wanaishi na VVU. Aidha, inakadiriwa kuwa takribani watu 1,548,000 wanaishi na VVU nchini, na kati yao watu 1,517,040 wanapata dawa za kufubaza VVU katika vituo vinavyotoa huduma hizi katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, utafiti huo unaonyesha kuwa kiwango cha wateja waliofubaza virusi kwa kiwango kinachohitajika (yaani Viral Load Suppression) nchini Tanzania ni asilimia 94.3% kwa walio kwenye dawa.
Amref Health Africa nchini Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali, washirika, na wadau ili kufikia malengo ya mradi wa Afya Thabiti na kuongeza kasi ya kufikia malengo ya 95-95-95 ya kudhibiti VVU na UKIMWI nchini Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe Said Mohamed Mtanda wakati wa Uzinduzi rasmi wa mradi wa Afya Thabiti Mkoani Simiyu na Mara uliofanyika Simiyu.
Wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, wawakilishi wa wadau wa maendeleo (PEPFAR-CDC), wafanyakazi wa Amref Health Africa, asasi za kiraia, washirika wa utekelezaji, viongozi wa kidini wa kikanda, jamii, na sekta binafsi wakati wa Uzinduzi rasmi wa mradi wa Afya Thabiti Mkoani Simiyu na Mara uliofanyika Simiyu.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Dkt. Yahaya Nawanda (wapili kushoto) na mkuu wa mkoa wa Mara (wa kwanza kushoto) mara baada ya kuzindua mradi mradi wa Afya Thabiti Mkoani Simiyu na Mara uliofanyika Simiyu. Kushoto watatu Dkt George Mgomella mwakilishi kutoka Serikali ya Marekani CDC Tanzania, na mkurugenzi mkazi wa Amref Tanzania (wanne kushoto)
Social Plugin