Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Mwambungu akizungumza na waandishi wa habari
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Shinyanga, wameelezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Utawala wake namna alivyotoa Mabilioni ya fedha na kutekelezwa miradi mbalimbali.
Mafanikio hayo yameelezewa leo Machi 9,2024 na Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Mwambungu, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo.
Amesema Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Shinyanga wanahudumia Mtandao wa Barabara Kilomita 1,177.74, ambapo Kilomita 261.02 ni Barabara za Lami, na Kilomita 916.72 ni Barabara za Changarawe pamoja na Madaraja 309.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu cha Rais Samia tumepokea kiasi cha fedha Sh.bilioni 47.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na matengenezo ya barabara ili kufanya mtandao wa barabara uweze kupitika kipindi chote cha mwaka,”amesema Mhandisi Mwambungu.
Jitihada za Serikali kukabiliana na athari za Mvua za Elinino
Amesema Serikali kupitia TANROADS katika kuhakikisha Mvua hazileti madhara makubwa kwenye Sekta ya Miundombinu imetenga fedha za dharura Sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya matengenezo ya barabara, ambapo barabara zilizonufaika na mpango huo ni Kahama-Solwa Kilomita 79.96 na mawasiliamo yamerejea na inapitika vizuri.
Utekelezaji wa Miradi ya Kitaifa
Amesema wanasimamia mradi wa kitaifa wa ujenzi wa barabara Kiwango cha Lami Kilomita 50.3 kutoka Mwigumbi- Lamadi gharama ni Sh. Bilioni 72.2, Barabara ya Kagongwa- Bukooba hadi Nzenga Kilomita 66, Barabara ya Kahama- Kakola Kilomita 73 gharam Dola za Kimarekani Milioni 40 na Upanuzi Uwanja wa Ndege uliopo Ibadakuli Shinyanga gharama Sh.bilioni 49 na ujenzi upo asilimia 10.51.
Miradi ya Barabara iliyofanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kiwango cha Lami
Amezitaja Barabara hizo kuwa, ni Barabara ya Kolandoto-Lalago Kilomita 53 na upembuzi yakinifu na usanifu umekwisha kamilika kwa asilimia 100, Barabara ya Oldshinyanga-Salawe Kilomita 64.66, Barabara ya Uyogo, Nyamilangano,Nyandekwa hadi Kahama, na Kilomita 54 zipo Shinyanga hadi Kaliua na Mpanda.
Ametaja Barabara nyingine ni ya Oldshinyanga- Bubiki Kilomita 53, Barabara ya Kahama- Solwa Kilomita 76.69 ambayo ni Border ya Mwanza.
Usimikaji wa Taa za Mwanga Barabarani
Amesema kwa kipindi hicho cha utawala wa Rais Samia wamefanikiwa kusimika jumla ya taa 395 kwa gharama ya Sh. Bilioni 1.18 katika Miji na Vijiji vya Tinde, Isaka, Kagongwa, Kahama, Segese na Bulige pamoja na taa zitakazofungwa maeneo ya Vijiji vya Solwa na Ngaya.
“Namshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha nyingi mahususi kwa ajili ya Mkoa wa Shinyanga, ili kuifungua Shinyanga na kukuza uchumi kwa ujumla, pia ameendelea kuleta fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya Barabara ili zipitike kwa kipindi chote cha mwaka, na jumla ya Sh.bilioni 325 kwa miradi yote mikubwa na matengezo zimeletwa kwa miaka mitatu,”amesema Mhandisi Mwambungu.
Wito kwa Wananchi
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwamba waitunze miundombinu ya barabara zikiwamo alama za barabarani na pamoja na Taa, kutomwaga Mafuta kwenye Lami, Wasafirishaji kutozidisha uzito kwenye Magari, kulinda na kutovamia hifadhi ya Barabara.
Social Plugin